Habari

CBK yashikilia tafsiri sahihi ya 'Bank' ni 'Banki' kwenye noti mpya

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MKUU wa kitengo cha mawasiliano katika Benki Kuu ya Kenya Wallace Kantai (pichani) Jumatano alizima mjadala kuhusu lipi neno sahihi kati ya “Benki” na “Banki” kama ilivyotumiwa katika noti za Kenya, mpya na za zamani.

Mjadala mkali umekuwa ukiendelea miongoni mwa Wakenya mitandaoni kuhusu suala hilo huku wengi wakipinga matumizi ya “Banki Kuu ya Kenya” badala ya “Benki” kama ilivyotumiwa katika noti za taifa jirani la Tanzania.

Akijibu wito wa Shirikisho la Watumiaji Bidhaa Nchini (Cofek) kwamba noti za Kenya ziondolewe ili zichapishwe upya na kusoma, “Benki Kuu ya Kenya,” Bw Kantai alisisitiza matumizi ya neno “Benki” ni sahihi.

“Matumizi ya “Banki” yamekuwepo tangu 1966. Nani sasa anasema ni makosa?” Kantai akashangaa akiwajibu wakosoaji.

Bw Kantai alishikilia kuwa kauli za wataalamu wa Kiswahili na matumizi ya lahaja ya Tanzania hazipasi kutumiwa kama kigezo cha kubaini neno sahihi.

“Ningependa kuuliza Cofek hivi, je, mtandao wa Google ndio wenye usemi kuhusu lugha sahihi ya Kiswahili?” Bw Kantai akauliza.

Msomi wa Kiswahili Profesa Kimani Njogu, ambaye ni mmoja wa wataalamu waliotafsiri Katiba ya Kenya kwa Kiswahili, anasema kuwa tafsiri sahihi ya neno la Kiingereza “Bank” ni “Benki” kwa Kiswahili na wala sio “Banki”.

Hata hivyo, katika kamusi nyingi za Kiswahili, neno ‘Banki, lina maana sawa na ‘Benki’. Lakini wapenzi wengi wa Kiswahili hushikilia kuwa neno ‘Benki’ linafaa zaidi.

Neno ‘Banki, lina maana sawa na ‘Benki’, lakini wachanganuzi wa lugha ya Kiswahili husema neno ‘Benki’ ni sahihi zaidi.