Habari

Chaguzi ndogo kufanyika Isiolo, Embu na Kakamega Februari 26, 2026

Na NDUBI MOTURI December 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza Februari 26, 2026, kuwa siku ambayo chaguzi ndogo zitafanyika katika kaunti za Isiolo, Embu na Kakamega ambako viti vya uwakilishi vilisalia wazi.

Kupitia notisi, IEBC ilisema uchaguzi mdogo utafanyika eneobunge la Isiolo Kusini pamoja na viti vitatu vya udiwani katika wadi za Muminji na Evurore (Kaunti ya Embu) na Kabras Magharibi (Kaunti ya Kakamega).

Kiti cha Isiolo Kusini kilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Mohamed Tubi, aliyechaguliwa mwaka 2022 kwa tiketi ya chama cha Jubilee.

Viti vitatu vya udiwani vilibaki wazi baada ya waliokuwa wakivishikilia kujiuzulu ili kuwania ubunge.

Katika Mbeere Kaskazini, diwani wa wadi ya Muminji Newton Kariuki, aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Devolution Empowerment, na mwenzake wa Evurore Duncan Mbui walijiuzulu ili kugombea kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwezi jana.

Katika Kaunti ya Kakamega, diwani wa Kabras Magharibi David Ndakwa, aliyekuwa amechaguliwa kwa tiketi ya UDA, alijiuzulu kuwania kiti cha ubunge cha Malava, ambapo aliibuka mshindi.

IEBC imeweka ratiba kali ya maandalizi ya uchaguzi kuanzia mapema Januari. Vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki vimetakiwa kuwasilisha ratiba za kura za mchujo na orodha zilizoidhinishwa za wanachama ifikapo Januari 2, 2026, pamoja na majina na sahihi za maafisa walioidhinishwa kufikia Januari 13.

Vyama pia vinatakiwa kukamilisha kura za mchujo, kutatua migogoro yote ya ndani na kuwasilisha majina ya wagombeaji wao ifikapo Januari 16.

IEBC ilisema wagombeaji huru hawapaswi kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa angalau miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi mdogo, na wanatakiwa kuwasilisha majina na alama zao ifikapo Januari 2.

Uteuzi wa wagombeaji utafanyika Januari 22 na 23, huku kampeni zikianza Januari 22 na kukamilika Februari 23, siku mbili kabla ya uchaguzi.

Shughuli za kampeni zitaruhusiwa kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na mbili jioni.

IEBC ilisema itatumia sajili ya wapiga kura iliyothibitishwa Juni 21, 2022, katika uchaguzi mdogo za wadi kaunti za Embu na Kakamega, huku zoezi la usajili wa wapiga kura katika Isiolo Kusini likisitishwa hadi Machi 30, 2026