Chebukati: Familia kufichua kiini cha kifo chake baada ya kushauriana na madaktari
FAMILIA ya aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeahidi kutoa maelezo kuhusu kiini cha kifo chake baada ya kufanya mashauriano na madaktari waliokuwa wakimhudumia katika Nairobi Hospital.
Kwenye kikao na wanahabari, Ijumaa Februari 21, 2025 katika hifadhi ya maiti ya Lee Funeral Home, Nairobi, msemaji wa familia Eric Nyongesa Wafula aliomba wapewe muda na utulivu wakati huu.
“Alikufa Alhamisi mwendo wa saa tano za usiku katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akipokea matibabu kwa muda wa wiki moja. Wakati huu, kama familia hatuna mengi, kwani tunapanga kukutana na madaktari wake ili tufahamishwe kiini cha kifo chake ndiposa tuamue ikiwa maiti yake ifanyiwa upasuaji au la,” akaeleza Bw Wafula.
Aliandamana na mwana mkubwa wa Bw Chebukati, Jonathan Chebukati na kitinda mimba wake Emmanuel Chebukati na watu wengine wa familia.
“Tunaomba wanahabari na Wakenya wengine watupe muda wa kuomboleza kwa utulivu na kesho jioni tutaweza kutoa maelezo zaidi kuhusu kiini cha kifo chake na mipango itakayofuata,” Bw Wafula aliwaambia wanahabari.
Bw Chebukati, 63, alikufa Alhamisi usiku akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.
Aliteuliwa mwenyekiti wa IEBC mnamo Januari 17, 2017 kwa kipindi cha miaka sita.
Alichukuwa nafasi hiyo baada ya kuondolewa kwa aliyekuwa mwenyikiti wa tume hiyo Isaack Hassan ambaye sasa ndiye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kufuatilia Utendakazi wa Maafisa wa Polisi (IPOA).
Kabla ya kuteuliwa mwenyekiti wa IEBC Chebukati alikuwa akiendesha shughuli zake za uanasheria mjini Mombasa.
Lakini mnamo 2007 alijitosa kwenye ulingo wa siasa kwa kuwania kiti cha ubunge cha Saboti kwa tiketi ya ODM lakini akabwagwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.
Rais William Ruto amewaongoza viongozi wa matabaka mbali kumwomboleza Chebukati akimtaja kama kiongozi mwenye msimamo na aliyehudumia taifa kwa audilifu na moyo wa kujitolea.
“Nimepokea habari kuhusu kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kwa huzuni kubwa. Taifa limepoteza pakubwa kufuatia kifo cha Bw Chebukati ambaye alihudumu kwa uadilifu mkubwa,” Rais Ruto akasema.