Corona yachangia uhaba wa damu katika hifadhi Mombasa
Na MISHI GONGO
KUNA upungufu mkubwa wa damu katika kituo cha hifadhi ya bidhaa hiyo mjini Mombasa hali hii ikishuhudiwa tangu kuzuka kwa ugonjwa wa Covid-19.
Kulingana na mkuu wa hifadhi hiyo Bw Hamisi Kifi, hali hiyo inatokana na kusitishwa kwa shughuli za kukusanya damu kutoka kwa wakazi wa kujitolea mitaani kama mbinu ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.
Bw Kifi alisema tangu kisa cha kwanza kitangazwe nchini Machi 13, 2020, maafisa wa vituo vya kuhifadhi damu walisitisha mazoezi ya kukusanya damu kutokana na serikali kupiga marufuku ya kukongamana.
Akizungumza katika afisi za Huduma Centre mjini humo Ijumaa wiki jana katika shughuli ya kwanza ya kukusanya damu nje ya kituo chao tangu kuzuka kwa ugonjwa huo, Bw Kiti alisema ni muhimu kuchukua hatua za haraka kutatua uhaba wa damu katika kaunti hiyo.
Shughuli hiyo iliandaliwa na shirika la kijamii la Christian for Human Rights na hifadhi ya damu ya Mombasa.
“Wanafunzi wa shule za upili ndio wamekuwa wakichangia pakubwa katika utoaji wa damu, lakini tangu shule kufungwa na serikali ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, hifadhi yetu imepata pigo kubwa,” akasema.
Bw Kifi alisema nchini kuna upungufu wa painti 300,000 za damu.
“Tunastahili kuwa na painti 500,000 lakini kwa sasa tuna painti 200,000 pekee,” akasema.
Alieleza kuwa kwa sasa wanategemea familia kuchangia wagonjwa wao damu kufuatia uhaba ulioko kwa sasa.
“Kwa sasa tunategemea familia, lakini kuna matukio mengine ambayo familia haiwezi kusaidia. Kwa mfano, kwa wagonjwa wa sickle cell, familia inamchangia damu leo lakini baada ya wiki mbili anahitaji damu tena. Hii ikitokea watu waliomchangia hawatakuwa na uwezo wa kumfaa tena,” akasema.
Alisema wameanza mikakati ya kuchangisha damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu kwa dharura.
“Ugonjwa wa Covid-19 hautaondoka leo; hivyo tunatakiwa tufanye kwa umakini mkubwa,” akasema.
Aidha alisema kuekwa marufuku ya kuingia na kutoka kwa baadhi ya kaunti pia kumekuwa changamoto kwao kwani familia kutoka kaunti zingine za Pwani ambao wagonjwa wao wako katika hospitali kuu ya eneo la Pwani wanashindwa kuwachangia damu wakihitaji.
“Kuna muda nimelazimika kuandika barua ili kuwezesha jamaa kutoka Kaunti ya Kilifi kuingia Mombasa kuja kumchangia mgonjwa wake damu,” akasema.
Alisema uhaba wa damu pia umekuwa pigo kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezwa viwango vya juu vya damu.
“Baadhi ya wagonjwa wapaswa kufanyiwa upasuaji lakini kufuatia uhaba wa damu wanalazimika kusubiri. Hii inahatarisha maisha yao na pia kufanya ada za hosipitali kuongezeka kufuatia muda mwingi anaotumia kungoja,” akasema.
Mkuu huyo alisema kuna haja ya wakazi kuhamasishwa kuhusu umuhimu wa kutoa damu.
“Watu wengi huchangisha damu pale familia zao zinahitaji lakini wanadinda kushirika katika kutoa damu kwa misingi ya kuhifadhiwa na kuwafaa wengine,” akasema.
Aliwataja kina mama wajawazito,wagonjwa wa sickle cell, saratani na manusura wa ajali za barabarani kwamba wao ni kundi lenye uhitaji mkubwa wa damu.