Habari

Corona yapangua ibada, sadaka kutolewa kwa kutumia M-Pesa

March 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAITH NYAMAI

KWA mara ya kwanza katika historia ya Kenya, makanisa mengi yamesitisha ibada zao za Jumapili kote nchini na kuwaruhusu waumini kufuatilia ibada zao mitandaoni.

Haya yanajiri huku Kenya ikiweka mikakati kabambe ya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona ambavyo vimetangazwa kama janga la kimataifa.

Makanisa, badala yake, yameagiza wafuasi wake kukaa nyumbani na kuwataka kulipa zaka na sadaka zao pamoja na matoleo mengine kupitia M-Pesa na huduma nyinginezo za malipo kielektroniki.

Wale ambao hawajasitisha ibada zao wamegeukia kunyunyizia majengo ya makanisa yao dawa ya kuua bakteria na virusi.

Wengine wameahidi kutumia sabuni za kusafisha mikono, jeli na dawa za kuua viini kwenye mikono ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo miongoni mwa wafuasi wake.

Wahubiri wa Kanisa la Redeemed Christian Church of God Solution Centre Prince na Esther Obasike waliwaagiza wanachama wao kufuatilia ibada zao mtandaoni na kutoa nambari ya Paybill kwa wafuasi wao kulipa sadaka na zaka kupitia M-Pesa na huduma za mitandaoni.

Kanisa la Anglikana Kenya(ACK) pia limesitisha ibada zake zote za Jumapili kwa siku 30 zijazo kuambatana na amri ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kanisa hilo lilitangaza kwamba askofu Jackson Ole Sapit atakuwa akiongoza ibada maalum zitakazotangazwa Jumapili saa mbili asubuhi na Jumatano jioni.

Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA) pia limesitisha ibada zake za Jumapili na shughuli nyinginezo za kanisa kwa siku 21 zijazo kulingana na Katibu Mkuu wa PCEA, Mhubiri Peter Kaniah.

Kongamano la Maaskofu Wakatoliki Kenya lilisema misa zitaendelea katika makanisa yake yote lakini likasema limeweka mikakati ya kuhakikisha viwango vya juu vya usafi na umbali wa kutangamana kijamii wa mita moja vimezingatiwa.

Makanisa mengine ambayo yamesitisha ibada zake za Jumapili ni pamoja na Christ is The Answer Ministries (CITAM), Nairobi Gospel, City Church, Kenya Assemblies of God na mengineyo.

Katibu wa Kanisa la Africa Inland Church Kenya (AIC) Pasta John Kitala kupitia notisi kwa makanisa yake yote nchini, alisitisha mikutano yote ya ushirika na shughuli katikati ya wiki na kuwataka wafuasi kuzingatia umbali unaoruhusiwa wa kutangamana.

Kanisa la Redeemed Gospel la Askofu Arthur Gitonga lilisema limesitisha ibada zote na mikutano katikati mwa wiki, kesha lakini ibada za Jumapili zitasalia.

Apostle Julius Suubi wa Exploits Worship Centre alisema watanyunyizia makanisa yao dawa za kuua viini na kuwahimiza Wakenya kusimama imara kwa maombi.

Msikiti wa Jamia Nairobi pia ulisitisha ibada zake kufuatia amri ya serikali.