Dalili Rais Ruto alichezea shere Moi na Kanu
RAIS William Ruto anapoendelea kuimarisha mamlaka yake kabla ya uchaguzi wa 2027, minong’ono ya kusalitiwa imeanza kusikika ndani ya chama cha KANU, hali inayozua maswali mapya kuhusu hatima ya makubaliano ya kisiasa yaliyotarajiwa kurejesha familia ya Moi katika kitovu cha mamlaka ya kitaifa.
Ukimya wa Ikulu, ukosefu wa uteuzi katika nyadhifa serikalini na hali ya wasiwasi inayozidi kuongezeka ndani ya KANU imefufua mjadala kuhusu iwapo makubaliano ya kisiasa kati ya Rais Ruto na mwenyekiti wa Kanu, Bw Gideon Moi, yatatekelezwa kikamilifu au kama tayari yamesambaratika kimyakimya kutokana na matarajio ambayo hayajatimizwa.
Kilichotangazwa kuwa mkakati wa kurejesha Kanu kati serikali sasa kimegubikwa na hali ya sintofahamu.
Takriban miezi mitatu tu baada ya Rais Ruto kufanya ziara Kabarak, makao ya urithi wa kisiasa wa familia ya Moi, mashaka yanaongezeka kuhusu iwapo makubaliano hayo bado yapo hai au tayari yameporomoka.
Kando na kauli za ushirikiano zilizotolewa hadharani, kuna dalili za hasira ndani ya Kanu, huku maafisa wakuu wa chama hicho wakimlaumu Rais Ruto kwa kushindwa kutimiza ahadi zilizomshawishi Bw Moi kuacha azma yake ya kuwania kiti cha Seneti cha Baringo.
“Rais alituhadaa,” afisa mmoja mkuu wa Kanu aliambia Taifa Dijitali Jumanne, Januari 6, 2025 akiomba kutotajwa jina kutokana na uzito wa suala hilo.
“Hakukuwa na makubaliano ya maandishi, lakini Rais alitoa ahadi ya kutuingiza serikalini na kutupa nyadhifa. Kiongozi wetu hana furaha.”
Kwa mujibu wa afisa huyo, Bw Moi alichagua kwa makusudi makubaliano ya kuaminiana na hakushinikiza kuyaweka kwa maandishi.
“Gideon aliamua kumwamini Ruto kwa ahadi zake na hata akamwalika azungumze na wajumbe wa chama,” alisema.
“Sasa hakuna utekelezaji wowote. Hakuna dalili kwamba chochote kitatokea hivi karibuni.”
Kauli hii inaweka wazi wasiwasi unaoongezeka ndani ya Kanu, chama ambacho kilihisi kilikuwa kimeingia katika mkataba wa kisiasa wenye uzito kufuatia mazungumzo ya hadhi ya juu kati ya Rais Ruto na Moi Oktoba mwaka jana.
Matokeo yaliyoonekana zaidi ya makubaliano hayo yalikuwa kujiondoa ghafla kwa Bw Moi katika uchaguzi mdogo wa kiti cha Seneti kaunti ya Baringo, hatua iliyowashangaza wafuasi na wapinzani wake.
Wakati huo, wadokezi kadhaa viliambia Taifa Leo kwamba kujiondoa huko kulikuwa sehemu ya makubaliano mapana ambayo yangewezesha Kanu kujiunga rasmi katika Serikali Jumuishi kupitia uteuzi katika Baraza la Mawaziri, Makatibu na mabalozi.Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Kanu, Bw George Wainaina, amejaribu kutuliza tetesi kwamba makubaliano hayo yamekufa.
Alipoulizwa moja kwa moja iwapo yamesambaratika, alikataa kutoa kauli ya wazi.Pia alikanusha madai kwamba UDA ilidanganya Kanu ijiondoe katika kinyang’anyiro cha Baringo kisha ikakiuka ahadi zake.
UDA ya Rais Ruto imesisitiza kuwa ushirikiano huo bado upo. Mwenyekiti wa Kitaifa wa chama hicho, Gavana wa Embu, Cecily Mbarire, alisema kuchelewa huko ni kwa sababu za kiutaratibu, si za kisiasa.
“Tulifanya uchaguzi mdogo mwishoni mwa Novemba. Desemba ilikuwa fupi,” alisema.
“Tutaendelea baada ya chaguzi zetu za mashinani mwezi huu.”
Wachambuzi wa siasa wanasema mtazamo wa Rais Ruto kwa sasa umejikita zaidi katika kuimarisha chama chake, hali inayoweza kueleza kucheleweshwa kwa kupatia Kanu nafasi serikalini lakini wanaonya kuwa subira ndani ya kambi ya Moi inaelekea kuisha.
Makubaliano ya awali, kwa mujibu wa watu wa ndani, yaliwezeshwa kupitia ushawishi wa aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga na kukamilishwa rasmi baada ya mikutano kadhaa kati ya Rais Ruto na Bw Moi, ikiwemo mmoja uliofanyika Dubai.
Lengo lilikuwa kuashiria kurejea kwa Kanu katika kitovu cha mamlaka baada ya miaka mingi ya kutengwa kisiasa.