Habari

DCI yaanza kuchunguza kifo cha Prof Walibora

April 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

IDARA ya Upelelezi ya kesi za Jinai, DCI, sasa imeanzisha uchunguzi ili kubaini iwapo Profesa Ken Walibora alifariki kutokana na ajali ya kawaida.

Duru zilisema hatua ya DCI kutaka uchunguzi wa kina zilifanya mpango wa upasuaji wa mwili wake kuahirishwa Alhamisi.

Mwili wa msomi huyo maarufu sasa umepangiwa kufanyiwa upasuaji leo alasiri katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ili kufichua alivyofariki.

Hapo jana, mwili wa Prof Walibora ulihamishwa hadi katika kitengo cha watu mashuhuri katika mochari ya KNH huku familia ikishughulikia mipango ya mazishi.

Mnamo Jumatano, ilifichuka kwamba Prof Walibora aliaga dunia kutokana na majeraha mazito aliyoyapata baada ya kugongwa na basi la ‘Double M’ katika barabara ya Landhies, Nairobi karibu na kituo cha mabasi cha Machakos Country Bus.

Ilisemekana ajali ilitokea mnamo Ijumaa ya Aprili 10, 2020.

Lakini baadhi ya jamaa na marafiki zake wa karibu walitilia shaka habari hizo, baada ya gari lake jeusi aina ya Mercedes Benz kupatikana likiwa limeegeshwa kwenye barabara ya Kijabe, Nairobi, umbali wa takriban kilomita nne.

Gari hilo lilikokotwa hadi katika Kituo cha Polisi cha Central katikati mwa jiji la Nairobi ambapo duru zilisema polisi wa kitengo cha DCI walitarajia kulichunguza kwa kina.

Utata kuhusu jinsi Prof Walibora alivyohusika katika ajali alipokuwa akivuka barabara kwa miguu pamoja na kufikishwa KNH alikotibiwa na kuaga dunia baadaye bila kutambuliwa na yeyote, ni kati ya mambo yaliyozua shaka miongoni mwa jamaa na wandani wake.

Inatarajiwa baada ya uchunguzi kukamilika na mwili kufanyiwa upasuaji, mazishi yataandaliwa nyumbani kwao katika kijiji cha Makutano Kwa Ngozi, eneo la Cherangany, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Kutokana na masharti makali kuhusu usafiri kuzuia uenezaji wa virusi vya corona, mashabiki na wandani wake wengi walieleza masikitiko kwamba hawataweza kumpa heshima za mwisho inavyofaa mwandishi huyo anayefahamika zaidi kwa riwaya yake ya ‘Siku Njema’.

“Upasuaji ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya serikali na familia. Mbali na kuondoa shaka miongoni wengi, pia cheti cha daktari mpasuaji wa maiti (mwanapatholojia) kitasaidia familia kufuatilia masuala ya bima,” akasema Afisa wa Mawasiliano wa KNH, Hezekiel Peter Gikambi.

Bw Gikambi ambaye ni rafiki wa dhati wa marehemu, alizidi kusema: “Iwapo upasuaji utakamilika leo (Ijumaa) mapema, basi mwili wa Prof Walibora utasafirishwa hadi Cherangany kwa mazishi siku yoyote itakayoafikiwa. Sijaona haja ya pupa katika suala hili. Mwili wa Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Ndingi Mwana A’Nzeki ulihifadhiwa kwa muda kabla ya kuzikwa. Prof Walibora hakuaga dunia kutokana na corona ambapo angezikwa kwa haraka.”

Wakati uo huo, risala za rambirambi zilizidi kumiminika kutoka kwa wengi wa washairi, marafiki na wasomaji wa kazi mbalimbali za kifasihi zilizotungwa na Prof Walibora katika uhai wake.

Wanachama wa kikundi cha Wasomaji wa Taifa Leo (Wakita) kote nchini walieleza kupokea habari za kifo cha Prof Walibora kwa masikitiko, huzuni na majonzi makubwa.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wakita, Dkt Abdul Noor katika ujumbe wake alisema, “Ni masikitiko makubwa kwa wapenzi wote wa Kiswahili.”

Wanachama walisema watafanya mipango ya kutembelea familia ya Prof Walibora ili kuomboleza pamoja nao baada ya janga la corona kudhibitiwa vilivyo.

Mwandishi maarufu wa ‘Sauti ya Dhiki’, Abdilatif Abdalla alisema Walibora ameaga dunia wakati ambapo taaluma ya Kiswahili bado ilimhitaji mno.