Disaina matatani licha ya kurudisha mamilioni aliyotumiwa na NYS kimakosa
Na BERNADINE MUTANU
DISAINA mmoja wa fasheni za mavazi amejipata matatani katika sakata ya Huduma ya Kitaifa ya Vijana (NYS) kwa sababu ya ukarimu wake. Badala ya kumeza mamilioni aliyotumiwa kimakosa na NYS, fundi huyo wa nguo aliyarudisha.
Shirika la Utozaji Ushuru nchini (KRA) imemwendea Monica Kanari, mmiliki wa kampuni ya Occassions and Days Ltd, anayesemekana kupokea Sh15,306,689 asubuhi ya Desemba 20, 2016 katika hatua inayoaminika kuwa miongoni mwa ukora na wizi ulioendelea NYS.
Kanari alirudisha pesa hizo lakini badala yake akajipata katika orodha ya watu wanaoaminika kuwa wahusika wa sakata hiyo ambayo imepelekea kupotea kwa Sh9 bilioni.
Huyo ni Mkenya wa pili kukiri kupokea pesa kwa namna hiyo, baada ya Ann Ngirita, 30, kutoka Naivasha kusemekana kupokea Sh59 milioni kwa kuuzia NYS hewa.
Pesa hizo ziliwekwa katika Benki ya NIC kulingana na habari kutoka Benki Kuu ya Kenya na Wizara ya Huduma ya Umma na Vijana.
Baada ya kutambua kulikuwa na shida, Bi Kanari alimwandikia Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bi Lilian Omollo Desemba 23, 2016 kumtaka pesa hizo kurudishwa.
Sio wazi ikiwa katibu huyo alijibu barua hiyo. Disaina huyo alisema hakutuma ombi la kutoa bidhaa zozote NYS.
“Nimetoa maagizo kwa benki yangu kurudisha pesa hizo kwa akaunti 1000303301. Nituma ujumbe kuthibitisha kurudishwa kwa pesa hizo nikiupokea,” alisema katika barua pepe aliyomwandikia Bi Omollo.