Fujo serikalini zatisha kuyumbisha nchi
BENSON MATHEKA Na RICHARD MUNGUTI
MIZOZO ndani ya serikali ya Jubilee inatishia kulemaza nchi miaka mitatu kabla ya kukamilika kwa kipindi cha pili cha utawala wa Rais Uhuru Kenyatta na pia kuvuruga ugatuzi.
Huku Serikali Kuu ikikabiliwa na tofauti kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto, migawanyiko katika Baraza la Mawaziri na chama cha Jubilee, mitafaruku hiyo sasa imesambaa bungeni ambapo Alhamisi Seneti ilipeleka Bunge la Taifa kortini, siku tatu pekee baada ya magavana nao kwenda Korti ya Juu kutafuta ufafanuzi kuhusu mgao wa pesa kwa kaunti.
Suala hilo la mgao wa pesa kwa kaunti limeonyesha tofauti zilizopo kati ya Rais na Dkt Ruto licha yao kukanusha.
Hapo Alhamisi ofisi zao zililaumiana kuhusu barua iliyodaiwa kushauri Mwanasheria Mkuu, Paul Kihara kutafuta njia ya kisiasa kutatua suala hilo.
Duru zilisema Ikulu ilijitenga na barua hiyo ikisema afisa anayedaiwa kuiandika anahudumu katika ofisi ya Naibu Rais.
Mzozo huo umefufuta vita vya ubabe kati ya maseneta na wabunge, magavana na wabunge na serikali ya kitaifa na magavana.
Alhamisi jioni, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema ilikuwa ikichunguza barua hiyo.
Japo maseneta, ambao waliwasilisha kesi jana wanalaumu wabunge kwa kupitisha sheria 24 zinazohusu serikali za kaunti bila kuihusisha, chanzo cha mzozo huo ni hatua ya bunge kupunguza pesa zilizotengewa serikali za kaunti.
Fujo zilijitokeza zaidi baada ya mabunge yote mawili kuchapisha miswada tofauti Seneti ikiunga mkono Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kutengea serikali za kaunti Sh335 bilioni, nayo bunge la taifa likitengea serikali hizo Sh316 bilioni.
Maswali yameibuka kuhusu ushauri anaopata Rais, baada ya kubainika alitia sahihi mswada wa kuruhusu Serikali ya Kitaifa kutumia pesa za bajeti ya mwaka huu bila kufuata utaratibu unaofaa.
Kutiwa sahihi kwa mswada huo na mzozo kuhusu ugavi wa mapato kati ya seneti na bunge umefufua mizozo ambayo imekuwa ikitokota ndani ya serikali ya Jubilee na kuacha Wakenya wakiwa wamechanganyikiwa
Hii ni baada kuibuka kuwa unaweza kufanya shughuli za serikali kukwama kwa sababu jinsi hali ilivyo, serikali haiwezi kutoa pesa kutoka hazina kuu kufadhili miradi yake.
Hata hivyo, ikizingatiwa kuwa chama tawala kina idadi kubwa ya wabunge, maseneta na magavana, inaoneka serikali inakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kwenye kesi waliyowasilisha jana, maseneta wanalaumu Bunge la Taifa kwa kupitisha sheria 24 zinazohusu kaunti bila kuihusisha.
Sheria nyingine inayolengwa ni Sheria ya Afya inayofafanua jinsi ya kuthibiti ununuzi wa dawa zinazotumika katika hospitali za umma, usimamizi wa mamlaka ya taasisi za kutoa mafunzo ya tiba za afya (MTCs) miongoni mwa sheria nyingine.
Mnamo 2015 serikali ya kitaifa na magavana walitofautiana kuhusu hatua ya serikali ya kukodisha vifaa vya matibabu vya mabilioni ya pesa. Magavana walidai kwamba serikali ya kitaifa haikushauriana nao ilhali sekta ya afya imegatuliwa.
Huku mitafaruku ikiendelea ndani ya serikali na mabunge yote mawili, miradi ya maendeleo na shughuli katika viwango vyote vya serikali inakabiliwa na hali ya kukwama kwa kukosa pesa.
Kulingana na magavana na maseneta, serikali inakataa kutengea serikali za kaunti Sh335 bilioni ilhali ilitengea Ajenda Nne Kuu za Rais Kenyatta Sh451 bilioni ingawa ziko chini ya majukumu yaliyogatuliwa.
Wakiongozwa na Spika wa Seneti Keneth Lusaka maseneta 67 waliwasilisha kesi wakiomba kufutiliwa mbali kwa sheria 24 zilizopitishwa na bunge na kuidhinishwa bila mchango wao.