Habari

Tuliza boli! Gachagua na Kalonzo waumana ndimi

Na BENSON MATHEKA January 5th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

TOFAUTI zimeibuka kati ya kiongozi wa Democratic for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, na kinara wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, kuhusu wakati unaofaa kwa Muungano wa Upinzani kutangaza mgombea rasmi wa urais.

Bw Gachagua anasema upinzani haupaswi kuwa na haraka kutangaza mgombea wao kwa sasa akieleza kuwa kumtaja mapema kunaweza kumuweka katika hatari ya kushambuliwa kisiasa na serikali ya sasa.

Anasema jina la mgombea urais wa Muungano wa Upinzani linapasa kutangazwa “siku chache kabla ya uchaguzi,” akisema hii itawawezesha pia kuunganisha nguvu zaidi na vyama vingine vya kisiasa vinavyoweza kujiunga nao.

“Ikiwa tutafanya hivyo sasa, tunaweza kuwaacha nje watu kama ndugu yetu Edwin Sifuna( katibu mkuu wa ODM). Hata Mzee Oburu Odinga (kiongozi wa ODM) ameonyesha nia ya kuwania. Tunahitaji kuwasikiliza wote,” alisema.

Matamshi yake yalijiri siku chache baada ya Bw Musyoka kusema muungano huo umekubaliana kutangaza mgombea urais wake kufikia Machi mwaka huu.

Wiki jana, Bw Musyoka alisema upinzani kutangaza mgombea urais wake mwaka huu, kutatoa muda wa kutosha kwa muungano kukabiliana moja kwa moja na Rais William Ruto na kampeni zake.

Kulingana na Kalonzo, kutangaza mgombea urais wa upinznai mapema kutadhihirisha umoja na kujitolea kwa muungano huo dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

“Natoa ahadi hii kwenu: kufikia robo ya kwanza ya 2026, jina la mgombea wetu wa urais litafahamishwa kwa Wakenya. Muungano wa Upinzani si muungano wa kawaida tu; ni serikali yenu mbadala inayosubiri kuchukua hatamu. Tumeunganishwa si kwa tamaa binafsi, bali kwa misingi na maadili ya pamoja,” alisema Kalonzo katika ujumbe wake wa mwisho wa mwaka.

Alisema viongozi wa upinzani wamekubaliana kuwasilisha mgombea mmoja na hawana nia ya kuchelewesha maandalizi, akitaja shinikizo za wananchi wanaotaka mabadiliko.

Alieleza kuwa uamuzi wa kumtangaza mgombea kufikia Aprili 2026 utaondoa wasiwasi wa wafuasi kuwa vinara hawawezi kukubaliana.Akizungumza akiwa Murang’a Jumamosi, Bw Gachagua, alitofautiana na Bw Musyoka akisema ni mapema sana kumtaja mgombea urais wa upinzani.

“Mimi naomba tuwe na subira kuhusu mgombea urais wetu. Hatuwezi kumtaja mapema kabla ya 2027 kwa kuwa tutampatia Rais Ruto nafasi ya kumshambulia,” alisema.

Alisema historia imeonyesha kuwa upinzani ukitaja mpeperusha bendera mapema, huwa katika hatari ya kupondwa na walio mamlakani.Akizungumza katika eneo la Kigumo, Kaunti ya Murang’a, Gachagua alipuuza madai kuwa upinzani uko tayari kutangaza mgombea urais mwaka huu akisisitiza kuwa hatua hiyo itakuwa ya pupa na hatari.

Alitoa kauli hiyo wakati wa mazishi ya mama yake Mbunge wa Embakasi North, James Gakuya, marehemu Alice Wangari.

Gachagua,alisema upinzani unafaa kusubiri hadi karibu na uchaguzi kabla ya kumtangaza mgombea wake, akionya kuwa ukifanya hivyo mapema utaalika vitisho kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo aliwahakikishia wafuasi wa upinzani kwamba, Muungano wa Upinzani uko na nia ya kuteua mmoja wao kushindana na Rais Ruto.

“Tutakuwa na mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto. Naomba watu wawe na subira. Msiwe na haraka. Uchaguzi bado uko mbali,” alisema Gachagua.

“Tukimtangaza mgombea wetu sasa hivi, atatishwa na kunyanyaswa na Ruto. Hatuwezi kufanya hivyo. Sisi si wajinga.”

Aliwahimiza wafuasi wa upinzani wawe watulivu, akisisitiza kuwa siri na muda sahihi ni muhimu ili kumlinda mgombea wa upinzani dhidi ya hujuma za serikali.

Bw Gachagua alirejelea Uchaguzi Mkuu wa 2002, ambapo muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) ulimtangaza mgombea wake wa urais muda mfupi kabla ya uchaguzi.

Alikumbusha kuwa marehemu Rais Mwai Kibaki alitangazwa kuwa mgombea wa NARC Oktoba 14, 2002, siku chache kabla ya uchaguzi wa Desemba 27, na baadaye akamshinda Uhuru Kenyatta aliyekuwa akiungwa mkono na Rais wa wakati huo Daniel arap Moi.