Gladys Wanga: ODM imeiva kwa kufanya uchaguzi wa amani na itashinda urais 2027
CHAMA cha ODM kimesema kina imani kwamba kitashinda uchaguzi mkuu 2027 na kupuuzilia mbali mapendekezo ya kuunda muungano wa kisiasa.
Hii ni baada ya kuanza uchaguzi wa mashinani wa chama hicho kote nchini unaokusudiwa kuimarisha chama hicho cha chungwa.
Mwenyekiti wa kitaifa wa ODM, Gladys Wanga, alisema shughuli hiyo ilikuwa ya amani katika maeneo mbalimbali akitoa wito kwa vijana kupigia debe chama hicho kinachoongozwa na Raila OdingA kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
“Watu wetu walijitokeza kwa wingi na kuwachagua maafisa wa chama. Vitendo vya ghasia havikushuhudiwa popote,” alisema Bi Wanga.
Alisema, “Vijana wanatekeleza wajibu muhimu kuhakikisha chama chetu kinafahamika vyema hivyo basi maafisa wote wa vijana ni sharti wawalete pamoja vijana ambao ni wafuasi wa chama.”
ODM vilevile inategemea wanawake kuvumisha na kuimarisha chama hicho.
Bi Wanga alisema wanawake ni miongoni mwa watu wanaoshiriki uchaguzi kwa wingi na kuwahimiza kupigia debe chama cha chungwa.
Alitangaza ODM itarekebisha makosa yote ambayo huenda imetenda hapo awali ambayo yameyeyusha umaarufu wake katika baadhi ya maeneo.
Alitangaza vilevile kuwa kuwa chama hicho kwa sasa hakipo tayari kwa miungano.
Alisema iwapo kuna mipango ya kubuni muungano wa kisiasa, mazungumzo kuhusu hilo yatafanyika baada ya uchaguzi.
“Kwa sasa, kila mtu anapaswa kuimarisha nyumba yake binafsi kwa sababu hivyo ndivyo tunafanya,” alisema.