Grace Msalame kushtaki UG kwa kutumia picha zake kuvumisha utalii
Na WYCLIFFE MUIA
MPANGO wa serikali ya Uganda wa kugeuza wanawake wanene kuwa kivutio cha kitalii, umeingia doa baada ya mtangazaji Grace Msalame wa Kenya kusema atashtaki wasimamizi wa mpango huo kwa kutumia picha zake kutangaza kampeni hiyo.
Mashindano hayo maarufu kama ‘Miss Curvy Uganda’ yalizinduliwa mnamo Jumatano na Waziri wa Utalii wa Uganda, Godfrey Kiwanda.
“Tuko na wanawake warembo waliobarikiwa kwa unene na umbo la kutamanika. Mbona tusiwatumie kuimarisha sekta ya utalii,” alisema Waziri Kiwanda akizindua kampeni hiyo.
Alipokuwa akizindua mashindano hayo, Bw Kiwanda alisambaza mabango yenye picha ambazo Bi Msalame anadai ni zake, na kuwataka wanawake wa Uganda wenye umbo kama la Mkenya huyo kushiriki kampeni hizo ambazo shabaha yake ni kuvutia watalii kuzuru Uganda.
Katika taarifa yake Alhamisi, Bi Msalame alijitenga na mashindano hayo akisema yanadunisha hadhi ya wanawake na kuwa matumizi ya picha zake yamemkera sana.
“Nimeudhika sana kwa picha zangu kutumika kueneza dhuluma dhidi ya wanawake. Sikubaliani kamwe na dhana kuwa mwili wa mwanamke unaweza kugeuzwa kuwa kivutio cha kitalii,” alisema Bi Msalame katika taarifa yake kwa vyombo ya habari.
Mwanahabari huyo alisema matumizi ya mwili wa mwanamke kuvutia watalii ni ukiukaji wa haki za kibinadamu na akatangaza kuwachukulia wasimamizi wa mashindano hayo hatua za kisheria.
“Nimefanya bidii nyingi katika kazi yangu ili kulinda hadhi yangu na bila shaka nimeanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya wahusika wa mashindano hayo,” alisema Bi Msalame.
Hatua ya Wizara ya Utalii nchini Uganda kutumia picha ya Mkenya katika mashindano hayo imewakera pia raia wengi wa Uganda waliolalamika kuwa huko ni ‘kukosewa heshima’ na serikali yao.
“Ni aibu kwa Uganda kutumia picha ya mgeni katika mashindano ya ‘Miss Curvy Uganda’. Kwani hakuna wanadada walioumbwa vyema Uganda?” alilalamika Noah Kisemi, katika mtandao wa Twitter.
Mashirika ya kijamii ya wanawake nchini Uganda vilevile yameapa kuzima mashindano hayo yakisema kuwa yanadunisha hadhi ya mwanamke katika jamii.
“Hatua hii ni ya kuhalalisha dhuluma dhidi ya wanawake. Tumeshuhudia mara nyingi wanaume wakiwapapasa kwa lazima wanawake mitaani Uganda na hatutakubali vitendo hivyo kuidhinishwa kuwa vya kitalii,” alisema mwanaharakati Primrose Murungi wa Uganda.
Bi Msalame anatarajiwa kuanzisha shoo mpya katika runinga ya NTV, Kenya.