Afueni kwa wafugaji punda 2,000 wakichanjwa Kirinyaga kukabili Kichaa
KAUNTI ya Kirinyaga imewapa chanjo zaidi ya punda 2,000 ili kukabili mkurupuko wa kichaa ambacho kimeathiri ufugaji wa wanyama hao wa kubeba mizigo.
Shughuli hiyo iliongozwa na Idara ya Kilimo na Ufugaji na ililenga maeneo ambayo ni hatari zaidi ili kuzuia maradhi hayo kuenea.
Wiki mbili zilizopita, punda aliyekuwa na kichaa aliwauma mifugo kadhaa na watu, hatua iliyoibua wasiwawasi miongoni mwa wakazi.
Katika eneo la Mwea pekee, punda 1,500 walichanjwa. Mkurugenzi wa Idara ya Mifugo Dkt Catherine Malonzi alisema chanjo hiyo ilikumbatiwa kutokana na malalamishi ya wakulima na ni shughuli ambayo sasa itakuwa ikifanyika kila mwaka.
“Tumekuwa tukishuhudia mkurupuko wa kichaa na kudhibiti hali kisha kuzuia visa kama hivi, tuna chanjo ambayo itazuia kuenea kwa maradhi hayo,” akasema Dkt Malonzi.
Alisema punda hao hutekeleza wajibu muhimu katika safari hasa kwa wakulima wadogo wadogo wanaosafirisha bidhaa zao sokoni au nyumbani.
Alisema madaktari wanaowachanja punda hao watazunguka kaunti nzima hadi wahakikishe kichaa kimetokomezwa.
Wakulima ambao punda wao walichanjwa, Jumatatu, Machi 31, 2025 walishukuru kaunti kutokana na juhudi zake za kudhibiti ugonjwa huo.
“Kaunti imesikiza kilio chetu na ikachukua hatua. Chanjo hii inatolewa bure na hii imetusaidia sana,” akasema Mary Muthee kutoka Ndorome.
Mkulima mwingine na mfugaji wa punda Peter Murimi alishukuru utawala wa Gavana Anne Waiguru kwa kuipa kipaumbele maslahi ya wafugaji wa punda.
“Miaka yote kama mfugaji wa punda, sijawahi kuona chanjo kama hii ikitolewa. Ugonjwa wa kichaa umetusumbua na nashukuru kaunti kwa kujitokeza na kutusaidia kupitia chanjo,” akasema Bw Murimi.