Baada ya mafuriko, kiangazi chaanza kutorosha wakazi makwao
WAKAZI katika baadhi ya maeneo ya Kaunti ya Tana River, wameanza kuhama makwao kwa sababu ya kiangazi.
Eneo hilo ambalo mapema mwaka huu lilikuwa miongoni mwa sehemu za nchi zilizoathirika pakubwa na mafuriko, sasa limeanza kuathirika na ukosefu wa lishe na maji kwa matumizi ya wakazi na mifugo.
Hali hii hujirudia kila mwaka ambapo punde baada ya msimu wa mvua, joto jingi hufuata na kukausha mimea na vidimbwi vya maji.
“Hakuna nyasi kaskazini, na hata ile kidogo iliyobaki inasababisha migogoro kwa kuwa kuna zaidi ya mifugo 100,000 huko, kwa hivyo ni lazima tuhame ili kupata sehemu nyingine salama,” mchungaji mifugo aliyejitambulisha kama Farhan, akasema.
Farhan, 17, anaongoza kundi la wavulana sita wanaochunga ng’ombe 1,700, na hadi sasa wamesafiri zaidi ya kilomita 200 na anatazamia kusafiri kilomita nyingine 200 wanapotafuta malisho katika maeneo ya Tana Delta.
Ngamia na punda pia hupelekwa hadi Tana Delta, na kila kijiji wanachoingia, vidimbwi vya maji vilivyojaa wakati wa mvua sasa vimekauka, na malisho yamekauka na kusababisha uhamiaji zaidi kutoka vijijini.
Katika eneo la Assa-Kone, idadi ya mifugo imepita idadi ya wakazi.
Kulingana na Chifu Roba Racha wa eneo la Assa, eneo hilo limepokea zaidi ya mifugo 60,000, na linaendelea kupokea angalau 5,000 kila siku huku kiangazi kinapozidi.
“Vidimbwi viwili vya maji hadi sasa vimekauka, kilichobaki hakitaweza kuhimili idadi hii hadi katikati ya Desemba, tayari tuna kesi za migogoro kati ya wenyeji na wafugaji wageni,” alisema.
Chifu huyo alielezea hofu ya kuongezeka kwa migogoro huku rasilimali zikiendelea kupungua kila siku, akiomba hatua zichuliwe upesi kabla ya hali ishindwe kudhibitiwa.
Hofu yake inaelezwa pia na wakulima katika Tana Delta ambao mazao yao bado hayajakomaa mashambani.
“Kila inapofikia hatua hii, migogoro inakaribia kwa sababu wafugaji hawataruhusiwa kuingia katika maeneo ya kuhifadhi wanyamapori, hivyo basi wataamua kukaa karibu na mashamba yetu,” alisema mkulima, Bi Helidah Hamaro.
Kulingana na Bi Hamaro, wafugaji hao huwa hawaheshimu mazao yao na wanachukulia kama nyasi, hivyo wao huachilia mifugo yao kuingia mashambani usiku.
Kamishna wa Kaunti ya Tana River David Koskei alikariri kuwa asasi za usalama ziko katika hali ya tahadhari, na zinaratibu kamati za kudhibiti mizozo zinazoongozwa na wazee katika maeneo yenye taharuki ili kuhakikisha utulivu unasalia.
“Wazee wetu wana uwezo na wakulima pia wanashauriwa kufanya kila liwezekanalo kulinda mashamba yao na kutoa mwongozo salama kwa wafugaji kuhusu njia za kunyweshea maji mifugo wao,” akasema.