Mamia ya familia kwenye kibaridi baada ya bomobomoa kurejea tena Kayole
Mamia ya familia eneo la Riverside katika mtaa wa mabanda wa Soweto, Kayole, Nairobi zinalilia haki baada ya ploti walimoita nyumbani kubomolewa na tingatinga.
Waathiriwa, ambao kwa sasa wanalazimika kulala katika vibanda vilivyoezekwa kutumia mifuko ya plastiki na kupikia vyakula nje ya uwanja wanaomba asasi husika za serikali kuchunguza kisa hicho.
Akiongea na Taifa Leo Alhamisi, msemaji wa waathiriwa hao, Pasta Cardinal Muiruri alisema wakazi walishtukia tingatinga likimoboa majengo yao kwa madai walikuwa wamejenga katika kingo za Mto Ngong.
Ajabu ni kwamba zoezi la kubomoa nyumba na vibanda kukomboa kingo za mito jijini Nairobi lilifanyika mwezi Mei mwaka huu na kusitishwa baadaye.
Zoezi hilo lilikuwa likitekelezwa baada ya agizo la Rais William Ruto kwamba watu waondolewe kutoka kingo za mito kote nchini ili kuepusha vifo kutokana na mafuriko.
Katika Mpango huo, jijini Nairobi, mito inayosafishwa na kingo zake kukombolewa ni pamoja na Mto Nairobi, Mto Ngong sawia na Mto Mathare.
“Serikali ilipima urefu wa mita 30 kutoka Mto Ngong ndiposa watu waliopatikana wakiiishi katika eneo hilo walihama kwa hiari japo hawakulipwa fidia ya serikali ya Sh10,000 kwa kila mwathiriwa,” akasema Pasta Muiruri.
“Siku ya Jumatano wiki jana, tingatinga liliponda nyumba zetu huku wakazi wengi wakiwa kazini. Tunakadiria kupata hasara kubwa baada ya mali ya thamani ya pesa isiyojulikana kuharibiwa.
Kando na nyumba, shule mbili –Bahati Community Centre Secondary na Soweto Complex iliyojumuisha shule ya Msingi na ya Upili zilibomolewa.
Taifa Leo ilibaini kwamba watahiniwa waliosajiliwa katika shule hizo walihamishwa kufanya mitihani ya kitaifa katika vituo jirani.
Mwathiriwa mwingine, Bi Lucia Mwendwa, 58, ambaye hufuga nguruwe alisimulia jinsi alivyowapoteza mifugo 15 wakati wa kukurukakara za ubomozi na kubaki na nguruwe wawili!
Paliposimama jengo la kuabudu Mungu katika Kanisa la Legio Maria, tulipata misalaba miwili na chungu kimoja zikiashiria hata makanisa hayakusazwa.
Mhudumu na mshiriki katika kanisa hilo, Bw Levi Onyango alisema kila Jumapili hulazimika kuweka hema kuendesha ibada na kulibomoa kila baada ya ibada kumalizika.
Bw Onyango alisema kanisa hilo linakadiria kupata hasara ya zaidi ya Sh1 milioni kufuatia ubomozi siku huo.
“Viongozi wetu pia humcha Mungu. Siku moja watakuja kwetu kuabudu. Kuna umuhimu wa kuheshimu Nyumba ya Mungu. Hatupingi kubomolewa kwa nia njema ya mito yetu kufuatia athari za Tabianchi, hata hivyo, tunairai serikali kututengea sehemu ya ardhi tuhamie huko,” akahoji.
Kiongozi wa vijana, Bw Osin Otieno almarufu Waz alisema vijana wametelekezwa na serikali na kumrai kuangazia masuala ya vijana.
“Tumeachwa mahali pabaya hasa wakati huu wa mvua. Pia kuna utapeli na ufisadi serikalini ndiposa naomba maafisa waliohusika na pesa za waathiriwa wa ubomozi kuchunguzwa kwani hatujalipwa chochote,” Bw Otieno akahoji.
Akitoa hoja kwa niaba ya akinamama, Bi Tabitha Karimihuku akilia, alikosoa serikali ya Kenya Kwanza na kumkumbusha Dkt Ruto kuwa ni makosa kuwabomolea mama mboga nyumba zao kinyume na ahadi alizotoa wakati wa kampeni.
“Tulipimiwa umbali wa mita 30 kutoka kingo za Mto Ngong kufika palipo nyumba zetu lakini wiki jana, tingatinga lilibomoa nyumba umbali wa mita 215 bila sisi kupewa notisi wala sababu ya lengo la serikali,” Bi Karimi akasema machozi yakimtiririka kutokana na kumbukumbu ya siku hiyo.
Kadhalika, mwenyekiti wa Vuguvugu la Mapasta wa makanisa zadi ya 500 liitwalo Sauti Mashinani, na Mkuu wa kanisa la Jesus Restoration Centre, Askofu DKt Josphat Njoroge alisema kuna umuhimu wa serikali kuchunguza jinsi zoezi la ubomozi liliendeshwa na kukosoa akisema kulikuwa na siasa katika mchakato wa kubomoa nyumba.
“Ni jukumu la kanisa kuikosoa serikali. Hata mti ukikatwa, humea tena. Lazima maisha ya watu ambayo ni muhimu kuangaziwa na ni lazima maisha yaendelee. Kulikuwa na dosari wakati wa ubomizi kutokana na misingi ya kisiasa. Taasisi husika za serikali ichunguze sakata hio,” akasema Askofu Njoroge.
Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino aliambia Taifa Leo kwamba serikali ilipuuza maagizo ya mahakama kusitisha ubomozi na kuongeza kwamba atawasiliana na mawakili wake kuishtaki serikali.