Habari za Kaunti

Kitendawili mama mjamzito akifariki hospitalini muuguzi akidaiwa kujipa shughuli

Na RUTH MBULA March 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UCHUNGUZI umeanzishwa kubaini kilichosababisha kifo cha mwanamke mjamzito kabla ya kujifungua katika hospitali moja huko Kisii, kufuatia kilio cha familia na umma.

Familia ya Phanice Ratemo inasema alifariki Jumanne (Machi 18, 2025) kutokana na uzembe wa wahudumu wa afya katika zahanati ya Magena na wanataka haki itendeke kwa mpendwa wao.

Waziri wa Afya Kaunti ya Kisii (CEM), Ronald Nyakweba, aliambia Taifa Dijitali kuwa uchunguzi wa maiti utafanywa ili kutoa msingi wa uchunguzi zaidi.

“Familia imeomba uchunguzi wa maiti ufanywe. Baada ya uchunguzi huo, tutaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kilichosababisha kifo cha mama huyo,” alisema Bw Nyakweba.

Kwa mujibu wa familia, Bi Ratemo alipelekwa kwenye zahanati hiyo Jumatatu usiku (Machi 17).

“Muuguzi aliendelea kutuambia tuwe na subira kwa sababu muda wa binti yangu kujifungua ulikuwa bado haujafika,” mama yake Ratemo, Joyce Kwamboka, aliambia wanahabari.

Bi Kwamboka anadai kuwa muuguzi aliyekuwepo alikuwa akijishughulisha zaidi na mambo yake binafsi badala ya kumhudumia mgonjwa na aliendelea kuwaambia waendelee kusubiri.

“Muuguzi alisema kuwa binti yangu bado hakuwa tayari kujifungua na alipaswa kufanya mazoezi katika uwanja wa hospitali. Pia, alisema kuwa mimi si daktari na nilipaswa kuwaachia wafanye kazi yao, na kama kungekuwa na haja ya kumhamisha mgonjwa, wangefanya hivyo,” alisema Bi Kwamboka.

Hata hivyo, Bw Nyakweba alisema kuwa si vyema kumlaumu muuguzi bila ushahidi wa uzembe, kwani uchungu wa kujifungua ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu.

“Tusitegemee uvumi; tutachunguza kiini cha kifo hicho,” alisema Bw Nyakweba, akiongeza, “Uchungu wa kujifungua ni mchakato unaoweza kuchukua hata siku nzima, kwa hivyo muuguzi huwa anamfuatilia mgonjwa na kumpa msaada wakati wa kujifungua.”

Aliongeza kuwa wauguzi walijitahidi kuokoa maisha ya mgonjwa huyo, lakini hawakufanikiwa.

Kifo hicho kimezua hasira katika Kaunti ya Kisii huku Gavana Simba Arati akihakikisha kuwa juhudi zitafanywa ili familia hiyo ipate haki.

“Kama kifo kilitokana na uzembe, hatua zitachukuliwa na yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliana na mkono wa sheria,” alisema Bw Arati akiwa hospitalini.

Alitembelea hospitali hiyo baada ya ripoti za kifo hicho kusambaa.

Pia, alikanusha madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa serikali ya kaunti inajihusisha na propaganda badala ya kuchukua hatua kuhakikisha familia inapata haki.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba tumepoteza maisha, na kwa sasa, tunaipa pole familia wakati huu wa huzuni,” alisema Gavana.

Bw Arati alithibitisha kuwa mwanamke huyo alipokelewa hospitalini na wahudumu wa afya walimwandaa ipasavyo kujifungua.

“Muuguzi aliyekuwa akimhudumia mgonjwa huyo amesaidia kina mama wengi kujifungua. Si mgeni katika kazi hii na tunapaswa kutoa nafasi kwa uchunguzi ufanyike,” alisema Bw Arati.