Madaktari wakora wamulikwa maduka ya kuuzia dawa yakifungwa
MADAKTARI wakora katika Hospitali ya Rufaa ya Kijana Wamalwa, Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, wameangaziwa kwa kuwanyima wagonjwa dawa na badala yake kuwatuma kununua kwa bei ghali katika maduka ya kuuzia dawa.
Serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia sasa imeagiza kufungwa kwa maduka yote ya kibinafsi ya kuuzia dawa karibu na hospitali hiyo ya umma, baada ya kubainika kuwa idadi kubwa inamilikiwa na madaktari wanaohudumu katika vituo vya afya vya umma vilivyopo karibu, ikiwemo hospitali hiyo ya rufaa.
Waziri wa Afya na Usafi, Sam Ojwang, amesema hatua hiyo inanuiwa kudhibiti tabia mbovu ya wahudumu wa afya wanaowatuma wagonjwa kununua dawa kutoka kwa maduka yao ya kibinafsi.
Alisema baadhi ya wahudumu wanamiliki maduka ya kibinafsi ya kuuzia dawa au wanashirikiana na maduka ya kibinafsi yaliyo karibu kunyima wagonjwa dawa na kisha kuwatuma kununua katika maduka hayo, na kuongezea mzigo familia ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto kulipa bili za matibabu.
“Udanganyifu huu kwa wagonjwa na wanaowatunza umewasababishia kununua dawa kwa bei ghali kutoka maduka ya kibinafsi ilhali hospitali zina bidhaa za kutosha,” alisema Waziri wa Afya wa kaunti.
Hatua ya kupiga marufuku shughuli za vituo vya kibinafsi vilivyopo karibu na hospitali hiyo, imefuatia malalamishi tele kutoka kwa umma kuhusu wagonjwa kutumwa kununua dawa katika maduka ya kibinafsi huku madaktari husika wakidai kuna uhaba hospitalini.
Waliozungumza na Taifa Dijitali walisema dawa zinazouzwa katika maduka hayo ni ghali zaidi.
Walifichua inahitaji ‘kumjua mtu’ ili kupata dawa kutoka hospitali hiyo kwa bei nafuu.