Habari za Kaunti

Madiwani wavamia hospitali ya Nakuru War Memorial iliyoko kwenye zogo kali na kaunti

Na MERCY KOSKEI October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KUNDI La madiwani kutoka Bunge la Kaunti ya Nakuru Jumatano walivamia Hospitali ya Nakuru War Memorial wakitaka ifunguliwe baada ya Mahakama ya Rufaa kutoa amri mwezi uliopita.

Hospitali hiyo ilifungwa miezi minane iliyopita na licha ya amri saba kutolewa kwa serikali ya kaunti kuifungua, bado haijafanya hivyo. Uongozi wa kaunti umekuwa na uhasama mkubwa na usimamizi wa hospitali hiyo uliokataa jaribio la utawala wa Gavana Susan Kihika kuitwaa.

Madiwani ambao walikuwa wengi, walivunja kufuli langoni mwa Nakuru Memorial, kisha wakaanza shughuli za kusafisha kwa kukata nyasi na kufyeka vichaka.

Kiongozi wa Wengi na Diwani wa wadi ya Keringet William Mutai alisema uvamizi huo ulikuwa hatua ya mwanzo ya kuhakikisha kuwa shughuli hospitalini humo zinarejelewa jinsi korti ilivyoamrisha.

Diwani wa Menengai Magharibi Isaak Rottok naye alishutumu kaunti kwa kupuuza amri ya kaunti na kuendelea kufunga hospitali hiyo.

Alisema kuwa Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Nakuru ambayo inastahili kuwahudumia wagonjwa kutoka Nakuru na kaunti jirani, nayo imepuuzwa na haitoa huduma za kimatibabu jinsi ambavyo inatarajiwa.

Bw Rottok alisema kuwa wagonjwa ambao wanahitaji huduma za uchunguzi wa MRI wanalazimishwa walipe Sh10,000 jambo ambalo hawatalikubali. Alisema kuwa pia kufungwa kwa Nakuru War Memorial kumewaathiri wagonjwa ambao husafishiwa damu (dialysis), wengi wao sasa wakilazimika kusaka matibabu Eldoret, Nyandarua na Baringo.

Diwani huyo pia alidai kuna watu ambao walikuwa wakitaka Nakuru War Memorial ifungwe ili kitengo cha kuwahudumia wagonja binafsi kwenye Hospitali Ya PGH kinufaike.

“Tunataka county iheshimu amri ya korti na iruhusu hospitali ya Memorial iendelee na shughuli zake kama zamani. Hospitali ya Rufaa ya Nakuru sasa inatumiwa na watu wachache kujinufaisha kifedha,” akasema Bw Ruttok.

“Tunaiomba serikali kuu iingilie kati na kufanya uchunguzi ili wafisadi hao wakamatwe,” akaongeza.