Habari za Kaunti

Mikakati kuangazia migogoro kati ya binadamu na wanyamapori

Na JURGEN NAMBEKA August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Taita Taveta, Andrew Mwadime ameeleza nia ya serikali yake kutafuta Suluhu la kudumu la kushughulikia migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, kama njia ya kuwaepushia wakazi hasara, maafa huku wanyamapori wakitunzwa.

Akizungumza wakati wa kufanya mkutano afisini mwake, Mwatate, alipotembelewa na maafisa kutoka kwa Hazina ya Kimataifa ya maslahi ya wanyama(IFAW), Bw Mwadime alielezea kwamba Taita Taveta ilikuwa ikifanya mazungumzo kuhakikisha wanyamapori wanatunzwa.

Alisema kuwa alilenga kushirikiana na IFAW kushughulikia migogoro hiyo ambayo ilikuwa imechochewa sana na mabadiliko ya tabianchi.

“Wakazi wetu wanapigana na wanyamapori kila mara kwa sababu ya uhaba wa maliasili kama vile maji na chakula haswa wakati wa kiangazi. Kwa kupata njia mwafaka ya kushughulikia shida hii inayohangaisha wakazi wetu moja kwa moja, tunaweza kuwa na athari kubwa sana,” akasema Bw Mwadime.

Kwa mujibu wa Naibu wa Rais anayesimamia miradi ya dunia katika IFAW, Bw Jimmiel Mandima, pendekezo hilo huenda laikawapa wakazi manufaa mengi kwa kuhakikisha kuwa binadamu na wanyamapori wanaishi kwa amani.

Kulingana na Naibu wa Gavana Taita Taveta, Bi Christine Kilalo, ushirikiano huo huenda ukawasaidia wanawake na watoto wanaoishi karibu na mbuga za wanyama kwa kuwa wanakodolewa macho na athari kubwa ya kuvamiwa na wanyamapori.

“Kuzuia wanyama hao na kuwatengea sehemu za kupata raslimali na hata kusafiri kwao kutawaokoa akina mama na watoto. Akina mama wanasaka kuni na hata maji mapema na jioni. Migogoro hii imewaacha wengi mayatima. Ni bora tukiwa hata na hazina ya kushughulikia watoto wanaopoteza wazazi kutokana migogoro hii,” akasema Bi Kilalo.