Habari za Kaunti

Mshukiwa wa mauaji Narok afikishwa mahakamani

Na KNA November 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MSHUKIWA wa mauaji anayehusishwa na visa vya mauaji katika Mji wa Narok na viunga vyake amefikishwa mahakamani.

Musa Ole Sopia almaarufu Ololulunga anashukiwa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji yaliyotokea katika mji huo Septemba ambapo takriban watu kumi walifariki katika hali tatanishi.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya kamera za CCTV kuonyesha picha zake wazi akishiriki wizi.

Pia anadaiwa kunaswa na kamera akimumuua mwanamume mwenye umri wa miaka 55 raia wa Congo, ambaye alikuwa akifanya kazi kama mlinzi katika kituo cha kibiashara cha Ololulunga.

Mshukiwa huyo alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Narok Daniel Ngayo mnamo Jumatatu.

Hakimu aliamuru afanyiwe uchunguzi wa afya ya akili katika hospitali ya serikali kabla ya kufunguliwa mashtaka.

Hakimu pia aliagiza mshukiwa azuiliwe katika gereza la Narok hadi tarehe 26/11/2024, siku ambayo mshukiwa anatarajiwa kuwasilishwa tena kortini.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Narok Riko Ngare alisema polisi wana ushahidi wa kutosha kumhusisha mshukiwa na kesi za mauaji.

Bw Ngare amemtaja kuwa kiongozi wa kundi haramu lililokuwa likiwahangaisha wakazi mjini Narok.

“Tunaamini kuwa mshukiwa ni kiongozi wa genge la wahalifu ambalo limekuwa likiwahangaisha watu katika mji wa Narok na kituo cha kibiashara cha Ololulunga. Tayari tumewakamata watu wawili, ambao kesi zao ziko mahakamani. Tunashuku kuna wanachama wengine wa genge moja ambao bado wako huru,” alisema.