Habari za Kaunti

Msidanganywe, hakuna kafyu huku, polisi waambia wakazi wa Likoni

Na  KEVIN MUTAI October 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

Polisi wamewahakikishia wakazi wa Likoni, Mombasa, kuwa eneo hilo liko salama na hakuna amri ya kutotoka nje usiku iliyotolewa kufuatia tukio la usalama lililosababisha kifo cha afisa wa kaunti na polisi mmoja kujeruhiwa.

Katika taarifa aliyotoa Oktoba 30, 2026, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Pwani Ali Nuno alisema tukio hilo lilitokea Jumatatu, Oktoba 26, maafisa walipokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Alifichua kuwa bunduki aina ya AK-47 pia ilipotea wakati wa tukio hilo.

Bw Nuno alitaja tukio hilo kuwa la uhalifu na kusisitiza kuwa halimaanishi kuwa Likoni au eneo lote la Mombasa halina usalama.

Alisema maafisa wa usalama wameimarisha msako wakilenga kuwakamata waliohusika, kurejesha bunduki iliyopotea na kuhakikisha washukiwa wanafikishwa mahakamani.

Akijibu uvumi uliokuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuwekwa kwa amri ya kutotoka nje usiku, kamanda huyo alipuuza madai hayo na kusisitiza kuwa hakuna amri kama hiyo iliyotolewa.

‘Hakuna marufuku ya kutembea Likoni. Wananchi wanaofuata sheria hawataathiriwa kwa namna yoyote na operesheni za kiusalama zinazoendelea,’ alisema.

Aliwataka wakazi kuwa watulivu na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, akionya kuwa habari za kupotosha zinaweza kuzua hofu isiyohitajika.

Pia aliwashauri wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu usalama kupitia matangazo rasmi ya Huduma ya Polisi nchini.

Wakati huo huo, idara za usalama zimeimarisha operesheni Likoni na maeneo mengine ya Mombasa ili kuwatambua washukiwa na kurejesha utulivu.

Kwa mujibu wa Bw Nuno, operesheni hizo zinalenga kuwakamata waliohusika na tukio hilo, kurejesha bunduki iliyopotea na kuimarisha doria katika maeneo yaliyoathiriwa.

Alisema maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa katika eneo hilo kulinda maisha na mali ya wakazi.

Aliwataka wakazi wa Likoni na Mombasa kuendelea na shughuli zao za kawaida bila hofu, huku wakishirikiana na polisi katika kudumisha amani.

Pia aliwahimiza wananchi kutoa taarifa za kuaminika zitakazosaidia uchunguzi na kukamatwa kwa washukiwa.

‘Naahidi wakazi wa eneo hili kuwa tutatekeleza wajibu wetu kwa haki, bila upendeleo, kwa uthabiti na kwa kuzingatia ukweli,’ akaongeza.

Polisi wamesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa jamii na kuwafikisha wahusika wa uhalifu Mahakamani