Habari za Kaunti

Msiposoma shauri yenu, Gavana aambia vijana akigawa basari za Sh5,000

Na WINNIE ATIENO August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir, amewashinikiza vijana walioacha shule kurudi kumaliza masomo yao hadi kidato cha nne.

Bw Nassir aliahidi kwamba serikali yake itawapatia wanafunzi wote wa Mombasa basari ya Sh5,000 kwa wale wanaosomea shule za kutwa katika kaunti hiyo.

“Hamna sababu ya kutokwenda shuleni sababu kuna basari ambayo tunapeana kwa kila shule kutwa. Ni sharti kwenda shule hadi kidato cha nne. Ukimaliza kidato cha nne aidha unaweza kujiunga na chuo kikuu na au chuo anuwai,” aliongeza.

Gavana Nassir alimtaka kamishna wa kaunti kuanza kushika doria kusaka watoto ambao hawaendi shuleni na kuwachukulia hatua wazazi.

“Sababu elimu ni lazima kwa mujibu wa katiba yetu na sheria. Nawasihi mkumbatie masuala ya elimu kuanzia, shule za chekechea, msingi, sekondari na vyuo vikuu na anuia,” alisisitiza.

Bw Nassir alisema mradi huo wa basari hauna ubaguzi akiwasihi wanafunzi na wazazi kuikumbatia.

Alisema waliomaliza kidato cha nne na hawakufaulu kupata alama za kujiunga na vyuo vikuu watafadhiliwa na kupelekwa vyuo anuia kusomea taaluma mbali mbali katika mradi wa ‘Skills Mtaani’.

Aliwaonya wasichana dhidi ya kujiingiza kwenye anasa na ukahaba.

“Msifikirie kuuza miili yenu, badala yake tumieni akili kuwa wabunifu ili kujikimu. Mambo ya kuuza miili haisaidii, kwanini ufikirie mabaya badala ya mazuri? Ni hatari sana kuwa na dhana hizo,” alisema.

Vile vile aliwataka vijana walioajiriwa kama vibarua kwneye mradi wa ‘Mombasa Yangu’ kuwa na nidhamu kazini.

“Lazima muwe na nidhamu ndio mufanikiwe maishani, hata wale vijana wa Mombasa yangu, wale ambao watapewa kipa umbele ya kuajiriwa ni wale wenye nidhamu,” alisisitiza.