Mshukiwa wa wizi wa ng’ombe aponea kifo Narok polisi wakimwokoa
POLISI wa Kilgoris, Kaunti ya Narok wamemwokoa mwanaume wa umri wa makamo mikononi mwa wanabiashara wa mifugo waliojawa na hasira.
Mwanaume huyo alikuwa ameiba ng’ombe watatu kutoka kijijini Shartuka na alikuwa katika harakati ya kuwauza katika soko la mifugo la Kilgoris.
Maafisa wa usalama wa kaunti walimfungia mshukiwa katika ofisi zao za kukusanya mapato.
Wakati huu wanabishara wenye hasira walikuwa wanazingira eneo hilo.
Hapo ndipo maafisa wa polisi walifika na kumwokoa mwanaume huyo asiathiriwe na ghadhabu ya wanabiashara hao walioapa kumwangamiza.
Akizungumza kwa niaba ya wanabiashara, Bw Samson Lemayian, alieleza kuwa si mara ya kwanza kwa mshukiwa huyo kuiba mifugo.
Bw Lemayian anasema kuwa aliwahi kukamatwa kwa kosa hilo kisha akaachiliwa.
“Tunaomba polisi wachukue hatua kamili ya kisheria kwa sababu mshukiwa amezoea kutekeleza wizi,” alisema.
Mwanabiashara mwingine, James Nkiok, alikuwa na wasiwasi kuwa tukio hilo litawachafulia jina wanabiashara wa mifugo.
Bw Nkiok anahofu kuwa watadhaniwa kuwa wezi wanaoiba mifugo kisha kuwauza sokoni humo.
Kwa hivyo, wanabiashara hao wanaomba polisi wawafungulie mashtaka washukiwa ili iwe funzo kwa wengine wanaohusika na ujangili.
Kwa sasa mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilgoris uchunguzi ukiendelea.