Mzozo watokota kaunti za Machakos, Makueni zikizozania mpaka
MZOZO unatokota baada ya Kaunti ya Machakos kukataa agizo la Wizara ya Ardhi la kuhamisha sehemu ya jiji la Konza katika kaunti ndogo ya Kalama, Machakos hadi kaunti ya Makueni.
Akizungumza na vyombo vya habari Jumamosi katika afisi ya Gavana, Katibu wa Kaunti ya Machakos Dkt Victor Ndambuki alisema kuwa watafanya kila wawezalo kusitisha mchakato huo na hakuna ardhi ya Machakos itakayohamishwa.
Hii ni baada ya Idara ya Serikali ya Ardhi na Mipango ya Ardhi katika Wizara ya Ardhi, kupitia ilani ya ndani, kuelekeza kaunti ya Machakos kuhamisha rekodi za ardhi za Konza kutoka kwa sajili ya ardhi ya Machakos hadi sajili ya ardhi ya Makueni.
“Waziri amezingatia suala hili na kuagiza kwamba rekodi zote zilizotajwa zihamishwe hadi kwenye sajili ya Wote ifikapo Jumatatu Desemba 30. Zaidi ya hayo, Mratibu wa Usimamizi wa Ardhi wa Makueni anaelekezwa kukubali kupokea rekodi zilizotajwa hapo juu na kuwasilisha nakala kwa afisi hii,” inasema sehemu ya ilani ya ndani iliyotiwa saini na Bw Mohammed Maalim, katibu wa usimamizi katika Wizara ya Ardhi.
Hata hivyo, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior amepuuza hatua ya Kaunti ya Machakos. “Sisi pekee ndio hatuzushi wakati Taita Taveta inadai mji wetu wa Mtito Andei, Kajiado inatunyima maji, Machakos inaweka rekodi za ardhi yetu na kukasirika wakati hati hizo zinahamishiwa kwetu,” Bw Kilonzo alisema katika taarifa yake jana.
Alikuwa akimjibu Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti ambaye alikuwa ameanzisha kampeni kali ya kuzuia Makueni kukabidhiwa ardhi hiyo.
“Machakos haitaachilia hata inchi moja ya eneo lake kwa mtu yeyote. Serikali ya Kaunti ya Machakos itafuatilia suala hili hadi tamati yake kwa njia zote zinazopatikana ikiwa ni pamoja na kualika mashirika husika ya serikali ya kitaifa na kutumia njia za kisheria,” Bi Ndeti alisema Ijumaa.
Dkt Ndambuki aliwahakikishia wakazi wa Machakos kwamba wanapanga kupinga agizo hilo kupitia njia zote zinazowezekana na kufuata mfumo wa haki ipasavyo.Waziri wa Ardhi katika serikali ya Kaunti ya Machakos, Bw Nathaniel Nganga, alikariri kuwa hawatakubali mipango yoyote ya kubadilisha mipaka ya Machakos na kuitaka Wizara ya ardhi kusitisha mchakato huo na kuwaita washikadau wote kwa mkutano.
“Tunaitaka Wizara ya Ardhi kusitisha mara moja hatua hiyo hadi pale kikao cha mashauriano kinachohusisha wadau wote kitakapofanyika,” alisisitiza Bw Nganga.
Diwani wa Kalama Bw Musyimi Maeke kwa upande wake aliongeza kuwa ushiriki wa umma ulifanyika mwaka wa 2010 katika Kaunti Ndogo ya Kalama ambapo saini zilichukuliwa na watu wa Kalama wakachagua kuwa chini ya Kaunti ya Machakos.
Maeke alibainisha kuwa madhumuni ya ugatuzi ni kuleta huduma karibu na wananchi na itakuwa si haki kwa watu wa Kalama kutarajiwa kupokea huduma kutoka Makueni ambayo iko umbali wa kilomita 130 ilhali Machakos iko karibu zaidi. “Haikubaliki kulazimisha watu kufasiri kinyume na mapenzi yao kutafuta huduma mbali na makazi yao,” alisema Maeke.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA