Habari za Kaunti

Naibu Gavana aonya wakazi Lamu ikilengwa na mashoga na wasagaji

Na KALUME KAZUNGU April 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Gavana wa Lamu, Bw Mbarak Bahjaj amewataka wananchi kuwa macho, akidai kuwepo kwa shinikizo za eneo hilo kuingizwa kwenye ushoga na usagaji (LGBTQ+).

Akizungumza mjini Lamu wakati wa kongamano la Eid Baraza, Bw Bahjaj aliwasisitizia viongozi wa dini, wazee, akina mama na vijana kuwa ange na kutoruhusu upotovu huo kuiteka jamii yao.

Lamu ni kisiwa cha dini ya Kiislamu, idadi kubwa ya wakazi wakiwa ni kutoka jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni.

Akitaja Uchaguzi Mkuu ujao wa 2027, Bw Bahjaj alifoka kuwa tayari kuna viongozi fulani watakaowania nyadhifa mbalimbali, ikiwemo ugavana, ubunge, useneta, madiwani na wengineo, lengo lao kuu likiwa ni kuruhusu ushoga na usagaji usambae Lamu.

Aliwashauri wakazi kwamba wakati wakichagua viongozi, ipo haja ya kuwachunguza na kuwakagua kwa undani wawaniaji mbalimbali wa nyadhifa hizo na kuhakikisha wenye nia mbaya na kaunti ya Lamu hawachaguliwi kamwe.

Pia, alifichua kuwepo kwa mashirika fulani ambayo tayari kupitia uongozi wa Gavana Issa Timamy na yeye kama naibu wake, wameyafurusha Lamu kwa kujaribu kupenyeza ajenda za ushoga na usagaji wakitumia mbinu ya kijanja ya kuanzisha miradi ya kibinadamu.

“Nina ushahidi kwamba Lamu yataka kuingizwa kindakindaki kwenye LGBTQ+. Kuna mashirika yamejaribu kuleta harakati hizo kisiri kupitia wizara yangu ya afya. Utasikia wakisema wataka kusaidia mambo na kansa ya kizazi, mara Ukimwi (HIV/AIDS) na kadhalika. Kupitia uongozi wa Gavana wetu, Issa Timamy, tulishirikiana, tukasimama kidete kuyafurusha mashirika hayo eneo hili,” akasema Bw Bahjaj.

Aliwasisitizia wakazi kuwa waangalifu ifikapo 2027, hasa wakati wakimchagua gavana, akimtaja kuwa kiungo muhimu kwani huwa kilele cha kupitisha masuala yote yanayohusu kaunti na wananchi wake.

“Gavana akiamua LGBTQ itambae, hapa Lamu itakuwa nyingi. Hivyo muwe waangalifu wakati mkichagua hao viongozi. Kuna watu wataka kusimama ugavana na wanapigia debe ushoga na usagaji. Punde wakichaguliwa itakuwa fursa nzuri ya kuingiza Lamu kwenye utovu huo wa maadili kwa mapana na marefu, tupende au tukatae. Tukatae hila zao,” akasema Bw Bahjaj.

Aidha, aliilaumu jamii ya Lamu na Pwani kwa jumla kwa kuitelekeza taasisi muhimu ambayo ni madrassa.

Alisema imekuwa rahisi kwa watoto kupotoka punde wanapojiunga na shule mbalimbali na vyuo kwani hukosa misingi dhabiti ya dini inayopatikana kupitia madrassa.

Aliwasisitizia wazazi kutosahau na badala yake kuthamini ipasavyo madrassa.