Habari za Kaunti

Serikali ya Kitaifa kukarabati shule zilizoathirika na mafuriko

Na NEHEMIAH OKWEMBAH July 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Kitaifa imeamua kufadhili ukarabati wa shule zilizoathiriwa na janga la mafuriko mwezi Mei.

Awali, Rais William Ruto aliwataka wabunge kutumia fedha za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF) kukarabati shule hizo kwa sababu Wizara ya Elimu haina hazina ya kushughulikia majanga.

Mamia ya shule sehemu mbalimbali nchini ziliharibiwa na mafuriko huku shule za kaunti ya Tana River zikiathiriwa zaidi.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliyezuru shule na kambi za wakimbizi wa ndani kwa ndani (IDPs) katika kaunti ndogo ya Tana Delta, alisema kuwa wizara yake sasa imetenga fedha za kugharamia ukarabati wa shule zilizoathirika na kuhamisha zingine ili kufanikisha shughuli za masomo katika eneo hilo.

Alisema serikali ya kitaifa imejitolea kabisa kuzihamisha shule zilizoathirika na mafuriko katika Kaunti ya Tana River.

“Tumetenga fedha ambazo zitaongezewa kwa zile za NG-CDF ili kugharamia ukarabati wa shule zilizoathirika na mafuriko,” Bw Machogu akasema

Waziri huyo alikuwa ameandamana na katibu katika Idara ya Ustawi wa Maeneo Kame, Kelo Arsama na Mbunge wa Garsen Ali Wario.

Angalau shule 22 katika kaunti ndogo ya Tana Delta zilifunikwa na maji ya mafuriko kati ya miezi ya Aprili na Mei mwaka huu kufuatia mvua kubwa iliyoshuhudiwa.

Baadhi ya shule zingali zimeloa maji hali ambayo imeathiri masomo ya maelfu ya wanafunzi.

Kuhusu uhaba wa walimu katika eneo hilo, Waziri Machogu alisema walimu zaidi watatumwa katika shule zenye idadi ndogo ya walimu.

Aidha, alitoa wito kwa wazazi kuwapeleka watoto wao waliohitimu kidato cha nne katika Vyuo vya Mafunzi ya Ualimu kama njia ya kufadia idadi kubwa ya walimu wazaliwa wa maeneo mengine.

“Nimeona kuwa mnakabiliwa na uhaba wa walimu 297 na kama wizara tutawatuma walimu zaidi humu  ili kuziba pengo hilo. Elimu ndio kisawazishi cha kipekee na hivyo nawahimiza wazazi wa hapa Tana River kuwapeleka watoto wao vyuoni mwa mafunzo ya ualimu,” Bw Machogu akaeleza.

Kwa upande wake, Katibu Arsama alisema idara yake tayari imesambaza mabati ya ujenzi, vifaa vingi na chakula kwa wakazi walioathiriwa na mafuriko ili waanze maisha upya.

Naye Bw Wario aliishukuru Serikali ya Kitaifa kwa kutoa hakikisho la kuwahamisha IDPs hadi maeneo yenye miinuko ili wasiathirike tena na mafuriko.