Simanzi mtahiniwa wa KCSE akifariki katika hali tata Turkana
MTAHINIWA wa Mitihani ya Kitaifa ya Shule ya Upili (KCSE) amefariki katika hali tatanishi katika Shule ya Upili ya Turkana Talent, Kaunti ya Turkana.
Chanzo cha kifo cha John Ekalale kilichotokea Jumatano hakijabainika moja kwa moja huku familia yake ikilaumu usimamizi wa shule kwa kutotoa taarifa ya hali ya mtoto wao kwa wakati.
“Tunapokuwa na masalio ya karo sisi hupigiwa simu na walimu lakini wakati mtoto wetu ni mgonjwa, hatupokei simu,” akateta mjomba wa marehemu Francis Nangodia.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Turkana ya Kati Evans Ombui amesema uchunguzi unaendelea kufichua kilichojiri katika bweni la shule hiyo iliyoko Turkana ya Kati.
Mwalimu Mkuu Samuel Otieno aliripoti kuwa mwanafunzi huyo alikuwa mzima kiafya hadi alipogunduliwa akiwa katika hali mbaya.
Alifariki alipopelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Lodwar kwa matibabu.
“Niliwapa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nambari za mawasiliano za wazazi,” alisema kujibu malalamishi ya familia. “Sikukataa kuwaambia wazazi, ni DCI walinizuia wakisema watawasiliana nao kupitia chifu.”
Kwa masikitiko makubwa, wanafunzi wenzake wanafichua kuwa hali yake haikuwa nzuri alipopatikana katika bweni.
“Tulianza naye kidato cha kwanza ni tunahisi vibaya kwa kumpoteza kabla ya kumaliza kidato cha nne,” alifadhaika mwanafunzi mwenza Venile Lokaala.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan