Tume yachunguza iwapo chuo kikuu kipya kinastahili kujengwa Kiabonyoru
TUME inayosimamia Elimu ya Vyuo Vikuu Nchini (CUE) inachunguza ufaafu wa Shule ya Upili ya Kiabonyoru, eneobunge la Mugirango Kaskazini, kama eneo linaloweza kuanzishwa ‘Chuo Kikuu cha Nyamira’ jinsi alivyotangaza majuzi Rais William Ruto.
Ikiongozwa na Mkurugenzi, Profesa Mike Kuria, tume hiyo ilituma timu ya wataalamu wa ‘ngazi za juu’ mashinani kuhakikisha kuwa uamuzi muafaka unafanywa kuhusu suala hilo.
Mvutano huo umekuwa ukitokota kwa majuma kadhaa sasa ambapo watu 44, akiwemo Mbunge wa Mugirango Magharibi, Stephen Mogaka wameelekea kortini wakitaka tangazo la Dkt Ruto lifutiliwe mbali wakisema ni wajibu wa CUE kupendekeza maeneo yanayofaa kwa vyuo vikuu.
Wabunge kutoka Kaunti ya Nyamira wamegawanyika, huku kila mmoja wao akitaka chuo kikuu hicho kianzishwe katika maeneobunge yao mtawalia.
“Tulikuja kama CUE kuhakikisha kuna msingi thabiti kwa elimu ya chuo kikuu kwenye ardhi hii, katika taasisi hii na eneo hili. Tulikuja hapa wenyewe ili tuseme tumeona,” alisema Profesa Kuria.
Mkurugenzi wa CUE alisema kikosi chao kilijumuisha wajumbe wa ngazi za juu, wakiwemo wahandisi, wataalamu wa masuala ya fedha, na mawakili ili kuhakikisha wanafanya uamuzi unaofaa, japo CUE bado haijatangaza eneo lolote.
Timu ya CUE ilijumuisha Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kisii, Profesa Nathan Ogechi na mbunge wa eneo hilo, Joash Nyamoko.
Chuo Kikuu cha Kisii kinatekeleza jukumu la taasisi kielelezo katika uanzilishi wa chuo kipya.
“Tunaangazia (mapendekezo ya Chuo Kikuu cha Kisii) kwa makini ili kuhakikisha kuwa maamuzi, mapendekezo tunayotoa yanajikita kwenye ushahidi ambao tumekusanya kutoka hapa. Hata hivyo, tunahitajika na sheria kufuata michakato fulani,” alisema.
Wakazi kadhaa wa Mugirango Kaskazini walijitokeza katika eneo hilo la Kiabonyoru wakielezea matumaini kwamba chuo hicho kitaanzishwa hapo.
“Lengo letu sio tu kupata eneo bali pia kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaokuja hapa kutoka sehemu zote nchini wanapata kutambuliwa kutokana na ujuzi wao baada ya kufuzu,” alisema Profesa Kuria.
Alisema taasisi hiyo inayopangiwa kuanzishwa inapaswa kutoa elimu bora ili hata watu maarufu katika jamii wanaweza kuwapeleka watoto wao kusomea hapo akiungwa mkono na Profesa Ogechi.
Kimaeneo, Kiabonyoru ndio mlima mrefu zaidi katika Kaunti ya Nyamira na ndiyo chemichemi ya Mto Gucha unaobubujika katika Ziwa Victoria baada ya kupitia maeneobunge kadhaa katika Kaunti za Nyamira, Kisii and Migori.
Akipinga vikali, Bw Mogaka alisema “Uadilifu wa Tume upo hatarini kwa sababu ya kisanga kilichoshuhudiwa Kiabonyoru ambacho hakikupaswa kutokea. Tume inazuru sehemu zote zilizochaguliwa na hii inathibitisha msimamo wangu kwamba Rais hakupatiana chuo kikuu Kiabonyoru.”
Imetafsiriwa na Mary Wangari