Habari za Kaunti

Uharibifu wa kuta za kukinga bahari waibua hofu

Na KALUME KAZUNGU August 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UHARIBIFU wa kuta zilizojengwa kandokando mwa Bahari Hindi kuzuia maji kufikia makazi ya binadamu Lamu na Pwani kwa jumla umeibua wasiwasi kwa wakazi na wataalamu wa mazingira.

Wataalamu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi wamesema mabadiliko ya kina cha maji ya bahari na ongezeko la mawimbi ni sababu kuu inayoharibu kuta nyingi za kukinga maji ya bahari Pwani.

Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi, ambaye pia ni afisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA), Bw James Kamula, alisema mabadiliko hayo ya tabianchi sasa yameongeza gharama ya kutekeleza ukarabati wa ngome za kukinga maji ya Bahari Hindi kufikia makazi ya binadamu.

Katika visiwa kama vile Mkokoni, Lamu Mashariki, wakazi kila mara wamekuwa wakiililia serikali kuwakarabatia ngome yao iliyoporomoka miaka kadhaa iliyopita kufuatia dhoruba inayochangiwa na mawimbi makali na upepo baharini.

Mnamo Aprili 2024, ukuta uliokuwa ukijengwa Mombasa katika eneo la baharini linalopakana na Kona Kilifi uliporomoka na kusababisha kifo cha mtu mmoja.

Bw Kamula alisema wananchi wanafaa wazingatie kutunza mazingira yao ili kuepuka kuendelea kushuhudia uharibifu unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Pia, aliwataka wawekezaji wa kibinafsi kuzingatia sheria zinazofungamana na maeneo oevu kila wakati wanapojenga miradi yao karibu na sehemu zinazopakana na Bahari Hindi.

“Lazima wawekezaji wajenge kwa kuzingatia umbali wa mita 60 kutoka ufuo wa bahari na maeneo oevu. Ngome nyingi na majengo yaliyojengwa maeneo yasikostahili yameishia kuporomoshwa na nguvu za maji.

“Isitoshe, uharibifu wa mazingira unaochangia mabadiliko ya tabianchi ndio umefanya ngome nyingi kuharibika kila mara, hivyo serikali kuishia kutumia fedha nyingi kukarabati ngome husika,” akasema Bw Kamula.

Gavana wa Lamu, Bw Issa Timamy, naye alishikilia haja ya wadau kuungana na kutenga fedha za kutosha ili kutekeleza ukarabati na ujenzi wa ngome za baharini eneo hilo.

Kulingana na Bw Timamy, kutekeleza ujenzi wa ngome za baharini ni hatua ghali, akitaja kuwa Kaunti ya Lamu hupokea mgao kidogo kutoka kwa hazina ya kitaifa ambao hauwezi kukimu mahitaji, ikiwemo ukarabati wa kila mara wa ngome.

“Ni wazi mabadiliko ya tabianchi yameongeza gharama kwani ngome zinaharibikaharibika kila kuchao. Ombi langu ni kwamba wadau na serikali washikane ili kusaidia kuzikarabati hizi ngome zetu,” akasema Bw Timamy.

Kauli yake iliungwa mkono na Diwani wa Wadi ya Kiunga, Bw Omar Bwana, aliyeiomba serikali na wadau kuharakisha kuanzisha ujenzi wa ngome ya kukinga maji ya baharini kufikia makazi ya binadamu Kisiwani Mkokoni.

Licha ya ngome hiyo kuporomoka miaka kadhaa iliyopita, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kufikia sasa kuijenga upya.

“Twahitaji kati ya Sh40 milioni na Sh60 milioni kufanikisha ujenzi wa ngome yetu ya Mkokoni. Nimekuwa nikijadiliana na gavana wetu, Issa Timamy na wadau ili kuona kwamba mradi huo unatekelezwa,” akasema Bw Omar.

Mwaka 2016, serikali kuu ilitekeleza ukarabati na ujenzi wa ngome ya Kizingitini, Lamu Mashariki kwa kima cha Sh200 milioni.

Mbali na Kizingitini na kisiwa cha Lamu, ngome nyingine zilizokarabatiwa ni Ndau, Kipungani, Matondoni, Faza na viunga vyake.

Maeneo mengine ambako ngome zinakosekana ni Kiunga na Ishakani.