Viongozi wa UDA Homa Bay waahidi Ruto atavuna kura kama njugu 2027
VIONGOZI wa UDA Kaunti ya Homa Bay sasa wanasema ni Rais William Ruto amewaamrisha wahakikishe eneo la Luo Nyanza linamuunga mkono katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kauli hiyo inatokea wakati ambapo Rais Ruto na Kinara wa Upinzani Raila Odinga wameanzisha ushirikiano wa kisiasa, hatua iliyosababisha wandani wake kuteuliwa serikalini.
Maafisa wa UDA wakiongozwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero, mwenyekiti wa Kaunti ya Homa Bay Kennedy Obuya na Katibu Silas Jakakimba, aliyekuwa mbunge wa Rangwe na mwanasiasa Odoyo Owidi walisema Rais amewaagiza waanzishe kampeni kabambe ya kuhakikisha Waluo wanamuunga mkono mnamo 2027.
“Tutaongeza idadi ya kura ambazo Rais atajizolea hadi zaidi ya asilimia 60 hapa Homa Bay na tushinde viti vyote vinavyowaniwa,” akasema Bw Kidero.
Matamshi hayo yanatolewa wiki mbili tu baada ya Rais kuzuru Nyanza ambapo alichangamkiwa na wakazi huku viongozi wa ODM wakiwapiga kumbo wenzao wa UDA.
“Rais Ruto amewaleta Wakenya wote pamoja na kila mtu anastahili kuwa sehemu ya serikali,” akasema Bw Kidero.
Bw Kidero alisema kutekelezwa kwa miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo hayakupigia serikali kura ikiwemo Nyanza, inaonyesha kuwa Rais Ruto ana utu na anawajali Wakenya wote.
“Uteuzi wa mawaziri ulizingatia sana msingi wa kufuzu kwao ndiposa Wakenya wote walisherehekea. Ulikuwa uamuzi mgumu kwa Rais lakini akaufanya,” akaongeza Bw Kidero.
Alikuwa akiongea mjini Kendu Bay wakati wa mkutano wa wanachama wa UDA Homa Bay.
Gavana huyo wa zamani alisema asilimia 40 ya wapigakura Homa Bay ni wanachama wa UDA na wanalenga kutokomeza umaarufu wa ODM katika kaunti hiyo.
Bw Owidi naye aliwataka wakazi wa Luo Nyanza waendelee kuunga mkono utawala wa sasa kwa sababu ya maendeleo huku akisifu wanachama wa ODM kwa kukubali kufanya kazi na serikali ya Kenya Kwanza.
Bw Jakakimba naye alionyesha imani kuwa miradi yote ambayo imeanzishwa na Rais Ruto Nyanza itatekelezwa au kukamilishwa kufikia 2027.