Habari za Kaunti

Wafugaji Kajiado kuhamasishwa kuhusu mbinu za kisasa za kilimo

Na  STANLEY NGOTHO December 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAFUGAJI kutoka kaunti ya Kajiado waliopoteza mifugo wao kutokana na ukame mkali kati ya mwaka 2020-2023, wamesalia kuhangaika katika juhudi zao za kukumbatia kilimo mbadala kutokana na ukosefu wa maarifa.

Wakazi wengi katika Kaunti ya Kajiado ambao ni wafugaji waliachwa bila mifugo na kuathiri maisha yao ya kila siku. Kufuatia kilio na mahangaiko ya wafugaji hawa, Benki ya Dunia kwa ushirikiano na serikali ya Kaunti ya Kajiado, imeanzisha mradi wa kutoa elimu ya bure kwa jamii hiyo ya wafugaji.

Chini ya mpango wa Agricultural Value Chain Development Project (NAVCDP), wataalamu wa kilimo 175 wametia saini kandarasi ya kuwaelimisha wafugaji hao vijijini jinsi ya kukumbatia ufugaji wa kisasa unaojumuisha ufugaji wa mifugo, kilimo cha mimea, ufugaji wa kuku pamoja na ufugaji wa nyuki kama mbinu mbadala.

Wataalamu hao wa kilimo ambao wamepewa ajira ya muda na Benki ya Dunia, wameratibiwa kutoa ushauri nasaha utakaowafaa wafugaji hao kufanya maamuzi bila kushurutishwa kuhusu kilimo mbadala watakachokumbatia.

Kando na hayo, wataalamu hao watawapa wakulima hao rekodi za soko za mifugo pamoja na mimea.Mradi huu unanuia kupiga jeki ufugaji wa mifugo, ukulima wa mimea, biashara ya maziwa na ngozi na vile vile ufugaji wa nyuki hasa nyanjani.

Kando na ajira kwa wataalamu hao, Gavana Joseph Ole Lenku amesema mradi huo utasaidia pakubwa katika kukabiliana na madhara ya tabia nchi pamoja na kutosheleza mazao ya chakula nchini.

“Wakati umewadia wafugaji wa Kajiado kukumbatia kilimo biashara.Kaunti ya Kajiado ina nafasi kubwa kuzalisha mifugo na mimea na kupata mapato ya mamilioni,” alisema Bw Lenku wakati wa kuzindua mradi huo siku ya Alhamisi.

Aidha, Bw Lenku amekiri kuwepo na changamoto ya maarifa kwa baadhi ya wafugaji.

“Changamoto kubwa ya wafugaji wetu ni kukosa maarifa.Maafisa hawa wataishi na wakulima mashinani na kuwapa ushauri kukabiliana na tabia nchi. Kila baada ya miaka miwili wafugaji wanakabiliwa na kiangazi.Lazima tutembee na majira sasa,” aliongezea Bw Lenku.

Serikali ya Kaunti ya Kajiado imeahidi kuendeleza mradi huu baada ya ufadhili wa Benki ya Dunia kufikia kikomo. Kwa kawaida wakulima wengi kutoka Kajiado hufuga ng’ombe kama mbinu ya kujikimu kimaisha idadi ambayo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na vifo vilivyosababishwa na ukame wa muda mrefu.