Zogo Sakaja akitwaa usimamizi wa Hospitali ya Mama Margaret Kenyatta
KUHAMISHWA kwa usimamizi wa Hospitali ya Mama Margaret Kenyatta kutoka kwa Hospitali ya Rufaaa ya Kenyatta hadi serikali ya Kaunti ya Nairobi kumezua uhasama kati ya madiwani wa Kaunti ya Nairobi.
Mmoja wa diwani wa kaunti ameapa kumkabili vikali Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuhusu suala hilo.
Hospitali ya Mama Margaret Kenyatta ambayo ina vitanda 548 ilizinduliwa tena na Gavana Johnson Sakaja Ijumaa iliyopita.
Hafla hiyo ilizingirwa na ubabe mkali, huku polisi wakikabiliana na vijana ambao walikuwa na hasira.
Inadaiwa Gavana aliharakisha uzinduzi na kuweka hospitali hiyo chini ya usimamizi wa kaunti licha ya kupokea barua ya malalamishi.
Barua hiyo iliandikwa na Diwani wa Kariobangi Kaskazini John Munuve na pia kunakiliwa kwa Rais William Ruto.
Hoja kuu kwa mujibu wa yaliyomo katika barua hiyo ni kuwa wakazi ambao wanaishi katika mitaa ya mabanda inayozunguka hospitali hiyo wataumia kaunti ikisimamia hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa diwani huyo, huduma za kiafya kwa wakazi wa Korogocho, Kariobangi na kaunti zitadorora zaidi kama hospitali hiyo itasimamiwa na kaunti.
“Wakazi wa Kariobangi Kaskazini hawana imani na usimamizi wa kaunti kuendesha shughuli za hospitali hii. Mara nyingi hospitali za kaunti hukosa dawa, wauguzi, vifaa na mahitaji mengine mengi kwa wagonjwa,” ikasema sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo pia ilinakiliwa kwa Wizara ya Afya, KNH na Waziri wa Afya katika Kaunti ya Nairobi.
“Wakazi wa Kariobangi Kaskazini sasa wanataka usimamizi wa hospitali ya Mama Margaret Kenyatta irejeshwe kwa KNH na si kaunti. Hoja kuu ni huduma kwa wakazi wa Kariobangi Kaskazini na eneobunge la Embakasi Kaskazini kwa jumla,” ikaongeza barua hiyo.
Kupitia mahojiano na Taifa Dijitali, diwani huyo alisema kuwa wasiwasi wake ni kuwa hospitali zinazosimamiwa na kaunti zimekuwa zikitoa huduma duni za afya.
Baadhi ya hospitali za kaunti ambazo alizitaja ni Pumwani na Mama Lucy huku akishutumu Gavana Sakaja kwa kumakinikia tu ukusanyaji wa mapato badala ya kuimarisha huduma kwa raia.
“Hospitali ipo katikati mwa mtaa wa mabanda na wakazi hawatakuwa na pesa za kulipa kabla ya kuhudumiwa iwapo sasa itasimamiwa na kaunti,” akaongeza.
Hata hivyo, Afisa Mkuu Msimamizi wa Vituo vya Afya Nairobi, Geoffrey Mosiria alisema Bw Munuve anaingiza siasa kwenye huduma za afya.
Aidha, alisema kuwa huduma zitaboreshwa zaidi chini ya usimamizi wa kaunti.
“Kile ambacho diwani huyo anasahau ni kuwa kaunti ina jukumu la kutoa huduma za kiafya kwa wakazi wa Nairobi na si kucheza siasa,” akasema Bw Mosiria.
Wakati wa uzinduzi ambao ulifanyika Ijumaa, watu kadhaa walijeruhiwa mirengo miwili ilipopigana na kulazimisha polisi waingilie kati.
Bw Munuve alisema alizuiwa kushiriki hafla hiyo kwa hofu ya waandalizi kuwa angempinga Gavana Sakaja licha ya mkutano huo kuandaliwa katika wadi.