Afrika Kusini na Rwanda zakabana kuhusu vita DRC
KIGALI, RWANDA
RAIS wa Rwanda Paul Kagame amemchemkia mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na serikali yake akidai wanaeneza uongo kuhusu mzozo unaoendelea kutokota Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kiongozi huyo amesema Rwanda iko tayari kuenda vitani na Afrika Kusini iwapo uhasama huo utaendelea. Wapiganiaji wa M23 wameteka mji wa Goma mashariki mwa DRC na wamekuwa kwenye vita vikali na wanajeshi wa serikali.
Madai yamezuka kuwa Rwanda imekuwa ikifadhili M23 ili kuwa na udhibiti wa Goma na inufaike madini tele ili kujitajirisha. Utawala wa DRC nao umekuwa ukipambana ili eneo hilo liendelee kuwa kwenye himaya yake japo baadhi ya wakazi wake ni Watutsi ambao asili yao ni Rwanda.
“Kile ambacho kimesemwa kuhusu mazungumzo yetu na Ramaphosa wiki hii kimetiwa chumvi, si ukweli na kuna nia ya kuchochea vita. Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimekuwa vikisema uongo,” akasema Rais Kagame.
Kutokana na mauti ya wanajeshi 13 wa Afrika Kusini ambao wamekuwa wakisaidia serikali ya DRC kukabiliana na waasi wa M23, Rais Ramaphosa alielekezea kidole cha lawama Rwanda.
Afrika Kusini inadai wanajeshi wa Rwanda waliungana na M23 kuwaua wanajeshi wake ambao wapo kwenye mpango wa kudumisha amani DRC. Mpango huo ulioidhinishwa na mataifa ya Kusini mwa Afrika unafahamika kama SAMIDRC.
Hata hivyo, Rais Kagame amesema SAMIDRC haina nia ya kurejesha amani bali imekuwa ikishirikiana na jeshi la DRC kuwaua raia mashariki mwa taifa hilo.
Alishangaa kwa nini Rais Ramaphosa amebadili kauli ihali hapo awali alikuwa amekiri kuwa M23 haikuhusika na mauaji ya wanajeshi wa Afrika Kusini bali waliohusika ni wanajeshi wa DRC.
“Kama Afrika Kusini inataka kuchangia suluhu ya amani ni vyema lakini hawafai kuwa mstari wa mbele kwenye meza ya maridhiano. Iwapo wanaonelea makabiliano ndiyo yatafaa, Rwanda ipo tayari siku yoyote,” akaongeza.