Habari za Kitaifa

Amerika yakumbusha raia wake Kenya Septemba ni mwezi wa mikosi ya mashambulizi

Na BENSON MATHEKA na ELVIS ONDIEKI September 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ya Amerika imekumbusha raia wake nchini Kenya kuwa waangalifu ikisema kunaweza kutokea mashambulizi ya kigaidi.

Mwezi wa Septemba, unasema Ubalozi wa Amerika nchini Kenya, ni mwezi wa kumbukumbu za mashambulizi makubwa ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na shambulio la 9/11 nchini Amerika na shambulio la Septemba 21, 2013 katika jumba la kibiashara la Westgate  jijini Nairobi.

Watu  2,977 walikufa katika shambulio la Amerika,  huku 67 wakipoteza maisha katika shambulio la Westgate, Nairobi.

“Ingawa mashambulizi yanaweza kutokea wakati wowote, wasiwasi unaongezeka karibu na tarehe za kumbukumbu za mashambulizi ya awali ya kigaidi, kama vile Septemba 11, shambulio la Septemba 21 la Westgate,” ubalozi ulisema katika ushauri  uliotoa Septemba 13, 2024.

Vile vile, ubalozi unasema, kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa shambulio la Hamas nchini Israeli (Oktoba 7, 2023) inakaribia.

“Ubalozi wa Amerika mjini Nairobi unawakumbusha raia wa Amerika nchini Kenya kwamba wanapaswa kuwa waangalifu zaidi kutokana na hatari za ugaidi na utekaji nyara. Maeneo yanayotembelewa na raia wa Amerika na watalii jijini Nairobi na kwingineko nchini Kenya yanaweza  kulengwa na magaidi,” ulisema ushauri wa ubalozi.

Ubalozi huo unashauri raia wa Amerika kuendelea kuwa macho katika maeneo yanayotembelewa na watalii, kutathmini  mipango yao ya kibinafsi ya usalama, kufuatilia vyombo vya habari vya humu nchini, kuepuka maeneo ambayo maandamano yanafanyika na  kuepuka mikusanyiko ya watu.

Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya ulisisitiza ushauri wa Ubalozi wa Amerika.