Ataweza ‘kupapasa’ Mlima?
RAIS William Ruto, akiandamana na naibu wake Prof Kithure Kindiki, leo ameanza ziara ya Mlima Kenya kwa mara ya kwanza tangu Novemba 16 mwaka jana, 2024 huku hasira zikitanda miongoni mwa baadhi ya wakazi.
Hasira hizo zinahusishwa na hatua ya Rais kumng’atua mamlakani aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua mwaka jana.
Aidha, ziara hiyo inajiri siku chache tu baada ya Dkt Ruto kumfuta kazi aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi.
Hatua hiyo ya kumfuta Bw Muturi, vilevile ilichukuliwa siku chache tu baada ya Rais Ruto kutia saini mkataba wa ushirikiano na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Bw Muturi amekuwa akiisuta serikali kutokana na ongezeko la visa vya utekaji nyara, hasa vijana kiholela tangu mwaka jana.
Licha ya Rais kumteua Prof Kindiki, anayetoka Mlima Kenya kuwa naibu wake mahali pa Bw Gachagua, wakazi wameendelea kupinga serikali wakihisi kusalitiwa.
Wameonekana kushikilia msimamo huo huo hata baada ya Dkt Ruto kuwateua kuwa mawaziri viongozi watatu, wenye ushawishi wa kisiasa, kutoka eneo hilo.
Wao ni aliyekuwa Seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo (ICT) na Gavana wa zamani wa Nakuru Lee Kinyanjui (Waziri wa Biashara).
Ni kutokana na hasira hizo za wakazi ambapo wandani wa Rais Ruto wamekuwa wakizunguka kote katika kaunti za Mlima Kenya wakijaribu kuwatuliza kabla ya ziara hiyo ya siku tano inayoanza katika kaunti za Laikipia na Nyeri.
Dkt Ruto atakamilisha ziara yake Ijumaa, Aprili 4, 2025 katika kaunti za Tharaka Nithi, anakotoka Prof Kindiki na Embu, anakotoka Bw Muturi.
Leo, Jumanne atazindua na kukagua miradi mbalimbali katika mji wa Rumuruti, Laikipia Magharibi, mji wa Nanyuki, Laikipia Mashariki kabla ya kuelekea Narumoru katika eneobunge la Kieni, Nyeri.
Dkt Ruto atakabiliwa na kibarua kigumu kujibu maswali kuhusu ni kwa nini wandani wa Bw Gachagua walitimuliwa katika nafasi za uongozi wa kamati za Bunge la Kitaifa na Seneti.
Hii ni licha ya kwamba wanasiasa hao walichangia pakubwa ushindi wake katika uchaguzi wa urais wa 2022 kwa kampeni.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, mwenzake wa Kipipiri Wanjiku Muhia, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utangamano wa Kikanda, Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC) na Mbunge wa Embakasi Kaskazini aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Biashara, James Gakuya.
Nafasi za wabunge hao zilitunukiwa wabunge wandani wa Bw Raila katika kile kilichoonekana kama mpango wa kuipa nguvu Serikali Jumuishi iliyoundwa Julai 2024 kufuatia ghasia za vijana wa Gen-Z.
Mbali na kutimuliwa kwa Bw Gachagua baadaye Oktoba, ni baada ya kushirikishwa kwa wandani kadhaa wa Bw Raila serikalini kulikochafua kabisa mandhari ya kisiasa Mlima Kenya.
Dkt Ruto alilazimika kulikwepa eneo hilo kwa karibu miezi sita licha ya kwamba lilimpa zaidi ya kura milioni 2.6 zilizomwezesha kumshinda Bw Raila katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9,2022.
Hii ndiyo maana Rais ameamua kurejea huko na minofu ili kujaribu kuwashawishi wananchi waunge mkono utawala wake.
Rais Ruto anatarajiwa kuzindua na kukagua miradi ya thamani ya mabilioni ya fedha katika sekta za miundomsingi, nyumba, umeme, maji na viwanda.
Hata kabla ya ziara ya leo, wafuasi wa Bw Gachagua na wale wa Rais mnamo Jumapili, Machi 30 walipigana eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang’a.
Makundi hayo mawili yalipambana katika Kanisa la AIPCA Mwagu Gatanga baada ya gari lililomilikiwa na Diwani wa Kariara Gichobe Mbatia kuharibiwa na makundi ya vijana. Tukio hilo lilijiri wakati ambapo ibada ilikuwa ikiendelea.
Baada ya ibada, diwani huyo pamoja na Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu na Mbunge wa Gatanga, Edward Muriu ambao ni wandani wa Bw Gachagua, walimshutumu Mwakilishi wa Kike Betty Maina kwa kuwadhamini wahuni hao.
Bw Mbatia alisema wahuni hao ambao walijihami kwa mapanga na silaha butu walisafirishwa kutoka Nairobi.
Hata hivyo, Bi Maina alikanusha madai hayo akisema tukio hilo ni ubabe wa kisiasa kuelekea kura ya 2027.
Aliweka wazi kuwa alialikwa kanisani humo na askofu na alishangazwa kusikia kulikuwa na mtafaruku nje.