Butere Girls: Mchezo wa Cleopas Malala wazua joto
SERIKALI imelaumiwa vikali kufuatia hatua ya polisi kufanyia ukatili wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere ikakosa kuonyesha mchezo wao “Echoes of War”, katika Tamasha ya Kitaifa ya Nyimbo na Michezo ya Kuigiza Kaunti ya Nakuru.
Mashirika ya kutetea haki za kibadamu, wanasiasa na wataalamu wa masuala ya sheria wametaja kitendo hicho kama ukiukaji wa haki za kikatiba ya wanafunzi hao kujieleza kupitia sanaa.
Wanafunzi hao walihangaishwa kuelekea siku ya kuonyesha mchezo huo huku mwandishi na mwelekezi wake Cleopas Malala akipata agizo la mahakama lililopuuzwa na polisi.
Awali, serikali ilikuwa imepiga marufuku mchezo huo.
Jaji Mkuu Martha Koome alikuwa miongoni mwa waliolaani tukio hilo.
“Kilichotokea leo kinatutahadharisha kuhusu kiwango ambacho amri za Mahakama Kuu zinapuuzwa. Kukataa kutii amri za mahakama hakudhuru tu mamlaka ya mahakama, bali pia kuna hatari kubwa kwa utawala wa sheria, ambao ni msingi wa jamii yetu,” alisema CJ Koome.
Jaji Mkuu alisema kwamba jambo linalotia wasiwasi zaidi ni taarifa za matumizi ya nguvu dhidi ya watoto wa shule.
“Ni lazima tuheshimu Katiba inayolinda kujitolea kwetu kwa utawala wa sheria na utawala wa kikatiba. Kila upotovu kutoka kwa njia hii unadhuru imani ya umma kwa taasisi zetu na kuna hatari kwa demokrasia yetu,” aliongeza.
Waandishi wa habari, wanafunzi na umma walizuiwa kuingia katika Ukumbi wa Melvine Jones Academy, Nakuru, ambapo wanafunzi wa Butere walikuwa waonyeshe tamthilia yao.
Tofauti na siku nyingine ambapo ilikuwa wazi kuhudhuria, walikutana na upinzani kutoka kwa polisi waliokuwa na silaha kwenye lango kuu na kuwaambia waondoke na kusimama nje.
Saa moja na dakika ishirini asubuhi, wasichana wa Butere walifika na kupokelewa kwa shangwe na umma na wanafunzi wenzao waliokuwa wakisubiri kushuhudia tamthilia hiyo.
Wanafunzi walijitokeza jukwaani, wakaimba wimbo wa taifa, kisha wakaondoka kwa hasira na kutaka Bw Malala aachiliwe huru.
Malala alikamatwa usiku wa Jumatano, Aprili 9, 2025 akiwa nje ya shule ya Kirobon, Nakuru, akitembelea wanafunzi waliokuwa wakifanya mazoezi ya mchezo huo.
Shirika la kimataifa kutetea haki, Amnesty International, tawi la Kenya, limetaka Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) kuanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa wa polisi waliorushia wanafunzi hao vitoza machozi ili wasiigize mchezo huo wenye maudhui ya kisiasa.
“Maafisa wote wa polisi walioshambulia wanafunzi hawa wasio na makosa, pamoja na wakubwa wao, sharti waadhibiwe kwa kukiuka kanuni za utendakazi wa polisi na Katiba ya Kenya. Aidha, inasikitisha kuwa polisi waliwashambulia wanahabari kwa namna ambayo inaonyesha wazi kuwa serikali haiheshimu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari,” akasema mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Irungu Houghton, kwenye taarifa.
Naye Rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Faith Odhiambo alilaani polisi akisema kitendo chao kinakiuka haki ya watoto.
“Utawala unaotaka kuheshimiwa unapasa kuzuia visa vya kushambuliwa kwa watoto. Inasikitisha kuwa wanyonge kama hawa ambao wanapasa kulindwa ndio sasa wamegeuzwa walengwa wa ukatili wa polisi na mienendo yao kutumia mamlaka vibaya,” Bi Odhiambo akaeleza.
Alisema kuwa japo Wakenya wamevumilia dhuluma za maafisa wa polisi wasioheshimu sheria, watoto wanaoshiriki sanaa hawafai kulengwa.
Kwa upande wake, Shirika la Kimataifa la Wanasheria (ICJ), tawi la Kenya, liliwasuta maafisa wa polisi likisema ni kinyume cha kipengele cha 53 cha Katiba na Sheria ya Watoto ya 2022 kwa polisi kuzima wanafunzi wa Butere Girls kuwasilisha mchezo “Echoes of War”.
“Tunapongeza Mahakama Kuu katika uamuzi wake wa Aprili 9, 2025 uliodumisha haki ya kikatiba ya wanafunzi hao kuigiza mchezo huo katika mashindano ya kitaifa. Agizo hilo la mahakama ni kielelezo kuwa utawala wa kisheria una mashiko kuliko masilahi ya watawala,” akaeleza mwenyekiti wa ICJ-Kenya, Protas Soende.
Kwa upande wao, wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka walisema kitendo cha polisi kinaashiria kuwa serikali ya Kenya Kwanza ni ya kidikteta.
“Hii ni aibu kubwa. Mbona serikali hii ishambulie kwa vitoza machozi wanafunzi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Butere wanapojiandaa kuigiza mchezo “Echoes of War” katika Tamasha ya Kitaifa ya Michezo ya Kuigiza. Nawaomba Wakenya kuunga nami kukataa utawala huu wa kidikteta,” akasema kupitia ujumbe katika akaunti yake ya X.
Nao wabunge Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Geoffrey Wandeto (Tetu) na Karungu Thangwa – Seneta wa Kiambu walishinikiza kudhibiwa vikali kwa maafisa wa polisi waliohusika na vitendo hivyo.
“Demokrasia yetu inaweza tu kukadiriwa kwa misingi ya namna tunalinda watoto. Hii ndio maana tunasema sharti polisi hao wawajibikie maovu hayo,” Bi Wamuchomba akaambia wanahabari katika majengo ya bunge.
Shutuma sawa na hizo pia zilitolewa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Jaji Mkuu mstaafu David Maraga.
“ODM inalaani vikali polisi kwa kurushia wanafunzi vitoza machozi wakiwa katika tamasha ya michezo ya kuigiza. Mbona serikali inaogopa mchezo, “Echoes of War” ambao ni jazanda inayoakisi utawala mbaya? Hii ni ishara kuwa utawala huu umekosa mwelekeo,” akasema Bw Sifuna ambaye pia ni Seneta wa Nairobi.
Mjadala kuhusu kisa hicho pia ulipenyeza katika Bunge la Kitaifa baada ya Mbunge wa Butere Tindi Mwale kusaka taarifa kutoka kwa Wizara ya Usalama kuhusu sababu ya serikali kuzuia uwasilishaji wa “Echoes of War”
Wabunge Aden Keynan (Eldas), Doris Donya (Kisii) na Mohamed Zamzam (Mombasa) walimshutumu mwanasiasa Cleophas Malala, aliyesanii mchezo huo kwa “kuwatumia watoto kuendeleza ajenda yake kisiasa kushambulia serikali.”
Mchezo wa ‘Echoes of War’ ulioandikwa na Cleophas Malala (Seneta wa zamani Kakamega), uliopaswa kuonyeshwa na wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Butere katika Tamasha la Michezo ya Kuigiza la Kitaifa, umeibua hisia baada ya wasichana hao kugoma kuuonyesha.
‘Echoes of War’ unahusu mgogoro wa vizazi, mabadiliko ya kijamii, na athari za teknolojia, masuala ambayo ni ya kisasa na yanahusiana na hali ya kisiasa na kijamii nchini Kenya. Mchezo huu unaangazia mapambano ya vijana dhidi ya mifumo ya utawala inayotawaliwa na hasa jinsi vijana wanavyokutana na upinzani wanapojaribu kupinga hali ya kawaida.
Mustafa, mhusika mkuu wa mchezo, anawakilisha vijana wenye ujuzi wa kiteknolojia.