Dalili wakulima wa miraa, muguka kutabasamu wakielekea benkini kufuatia mikakati ya serikali
SERIKALI imeingilia kati kukinga wakulima wasikandamizwe baada ya kubuni mfumo wa kubaini bei ya miraa na muguka chini ya sheria za kudhibiti miraa 2023.
Kamati hiyo inayojumuisha wanakamati tisa imetwikwa jukumu la kubuni namna ya kuweka bei ya miraa na muguka inayoongozwa na mazingira ya soko, gharama ya uzalishaji na masuala mengineyo.
Wawakilishi wa kamati hiyo wanajumuisha miungano ya wakuzaji, wauzaji, Baraza la Magavana, Mamlaka ya Kilimo na Chakula, Wizara za Kilimo na Biashara.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Mithika, alisema ajenda yao kuu itakuwa kusuluhisha kero ya wakulima kukandamizwa na wafanyabiashara pamoja na serikali kupitia ada
Wakulima wamekuwa wakiteseka kutokana na bei duni kwa sababu ya mtindo ambapo wauzaji bidhaa hizo katika mataifa ya kigeni, walikuwa wanawatoza ada wafanyabiashara wa humu nchini kwa miraa ambayo haijauzwa.
“Huku bei zikistahili kudhibitiwa na mazingira ya soko, wakulima wa miraa na muguka wameteseka kwa muda mrefu kwa sababu ya tabia ya mabwanyenye katika biashara hii. Tutajitahidi kupanua masoko ili kuongeza idadi ya wateja wa miraa na muguka,” alisema Bw Mithika akizungumza na wanahabari baada ya kuchaguliwa.
Alisema Kamati hiyo itatafiti masoko ya humu nchini na ya kigeni, kutathmini gharama ya uzalishaji na ada za serikali.