Habari za Kitaifa

Duale kupanda miti, Soipan Tuya kulinda nchi kufuatia mabadiliko mapya ya Rais

Na SAMWEL OWINO July 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KATIKA mabadiliko nadra sana, Rais William Ruto amemteua Bi Soipan Tuya kama Waziri wa Ulinzi wa Baraza la Mawaziri badala ya Bw Aden Duale ambaye sasa atahusika na mazingira, mabadiliko ya hali ya hewa na hifadhi ya misitu.

Mabadiliko hayo yamo katika barua ya Rais kwa bunge akiomba mawaziri wateule kuidhinishwa.

Alipotaja nusu ya mawaziri wake Ijumaa, Rais Ruto alimteua Bw Duale kama Waziri wa Ulinzi huku akiteua Bi Tuya kuendelea kusimamia wizara ya Mazingira, Mabadiliko ya Hali ya Anga na Misitu.

Mawasiliano hayo ambayo yalishangaza Bunge yalipelekea wabunge hao kupiga kelele wakimtaka Spika kuripoti.

“Tuna shaka ikiwa hii ndio habari ya kweli. Nataka kuwaambia wenzangu kwamba mara hii, msasa wa wateule hawa hautakuwa kama kawaida, safari hii, kama mtu hafai na hana uwezo, tutamtupa nje, Bw Spika,” alisema Kiranja wa walio Wachache, Bw Junet Mohamed.

Mbunge wa Tiaty William Kamket alisema “Ulichosoma kinakinzana na kile ambacho Rais alitangaza, ningependa uthibitishe kwamba ulichosoma ndicho kilichowasilishwa na Rais.  Hata kama kiwango kinafaa kuwa cha juu kwa yeyote anayeteuliwa waziri, hauwezi kutarajia Rais kuteua malaika katika Baraza la Mawaziri. Bw Mohamed hafai kutishia kazi za wengine,” Bw Kamket alisema.

Bw Duale alitumia akaunti yake ya X  kusema anashukuru kwa kukabidhiwa wizara nyingine.

“Ninatazamia kuhudumu katika wizara mpya na kuhakikisha usimamizi endelevu wa mazingira, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kukuza uhifadhi kwa kupanda miti tena kwa bidii,” Bw Duale alisema.