EACC, ODPP wavutana kuhusu kusamehe aliyetumia vyeti feki vya elimu kupata kazi
MVUTANO unatokota kati ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi Nchini (EACC) na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) baada ya EACC kupinga mipango ya kumwondolea kesi mfanyakazi wa zamani katika kaunti ya Nairobi, kuhusiana na kughushi stakabadhi za elimu.
Kupitia nakala ya kiapo iliyowasilishwa katika korti ya kukabiliana na ufisadi Milimani, EACC ilisema hatua inayokusudiwa kumwondolea mashtaka Bw Gabriel Bukachi Chapia, siyo kwa maslahi ya umma, utendaji haki wala kuzuia matumizi mabaya ya mchakato wa sheria.
EACC vilevile ilisema mashahidi 14 wametoa ushahidi wao katika kesi hiyo huku shahidi pekee aliyesalia ikiwa ni afisi inayofanya uchunguzi kabla ya upande wa mashtaka kufunga kesi hiyo.
“Suala kuu kwenye kesi sio mzozo kati ya watu binafsi bali linahusu makosa bayana ya umma ambapo hatua ya kisheria ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha na kuendeleza haki na maslahi ya umma kikatiba,” alisema mpelelezi wa EACC, Daniel Tipape, katika nakala ya kiapo.
Hakimu Mkuu, C.N. Ondieki, aliahirisha suala hilo hadi Novemba 7, ili kupatia muda ODPP kuwasilisha majibu yao kuhusu ombi la kuondoa kesi hiyo.
Taasisi za DPP na EACC zimekwaruzana hivi majuzi kuhusiana na kuondolewa kwa kesi za watu maarufu ikiwemo kesi dhidi ya Waziri wa Vyama vya Ushirika, Wycliffe Oparanya, waziri wa zamani Najib Balala na Gavana wa Tharaka Nithi, Muthomi Njuki.
Katika uamuzi uliotolewa majuzi, hakimu wa Kitui aliruhusu kuondolewa kwa mashtaka dhidi ya watu tisa walioshtakiwa kwa kuiba Sh292.7 milioni zilizodhamiriwa mradi wa maji, akisema uamuzi wa DPP ulifaa.
Hakimu Mkuu wa Kitui, David Mburu, alisema DPP alitenda haki kwa kufuta mashtaka hayo kwa maslahi ya umma na kuepuka mchakato wa sheria kutumiwa vibaya.
Alisema DPP alithibitisha kuwa, ukarabati uliofanyiwa mifereji ya Mradi wa Kusambaza Maji katika Kiwanda cha Ngozi cha Kinanie, uliovutia mashtaka kadhaa dhidi ya washukiwa, ulifanywa kupitia ushirikishaji wa umma.
“Kwa mtazamo wangu, DPP ametumia mamlaka yake inavyofaa akizingatia maslahi ya umma, maslahi ya usimamizi wa haki na haja ya kuzuia na kuepuka mchakato wa sheria kutumika vibaya,” alisema hakimu.
Bw Bukachi alishtakiwa Novemba 6, 2020 akikabiliwa na madai 16 ya kughushi, kutoa maelezo ya uongo na kughushi stakabadhi feki ili kupata ajira.