Faith Odhiambo hatajiunga na jopo la kukagua deni, LSK yaambia Ruto
CHAMA cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) kimekataa uteuzi wa rais wake Faith Odhiambo kuwa mwanachama wa jopokazi huru la kukagua deni la Kenya, lilioundwa na Rais William Ruto kikisema ni kinyume cha katiba.
Chama hicho kilisema kwamba kuteua jopokazi hilo ni sawa Rais William Ruto kutwaa mamlaka ya ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kwa kutilia maanani Kifungu cha 229 cha katiba na tafsiri ya vifungu hivyo na mahakama, LSK ilisema, “ni maoni yetu kwamba kuundwa kwa jopo kazi hilo ni kinyume cha katiba.”
Bi Odhiambo pamoja na aliyekuwa mkurugenzi wa IMF Nancy Onyango, Prof Luis Franceschi, Philip Kaikai, Shammah Kiteme na Vincent Kimosop, Ijumaa waliteuliwa na Rais William Ruto kama wanachama wa jopokazi kuhusu Ukaguzi wa Deni la Umma.
Hata hivyo, LSK ilisema imeazimia kwamba “rais wetu au mwanachama wetu yeyote hatakubali uteuzi au kushiriki katika jopokazi lililoundwa na kiongozi wa nchi”.
“LSK, chini ya mamlaka yake kisheria, inamshauri Rais [Ruto] ajizuie kutwaa mamlaka ya Kikatiba ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kupitia agizo la rais na kuruhusu Mkaguzi Mkuu kutekeleza majukumu yake ya kikatiba,” Afisa Mkuu Mtendaji wa LSK Florence Muturi alisema.
Vile vile, LSK ilisema, afisi ya Usimamizi wa Madeni ya Umma, inayoongozwa na Mkurugenzi Mkuu katika Hazina ya Taifa, na kufadhiliwa na pesa za umma, inafaa kutoa maelezo kuhusu deni la umma kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kwa ukaguzi wa kitalaamu.
“Ni muhimu kutofuja rasilimali chache za umma kwa kuteua jopokazi kutekeleza majukumu ya ofisi zilizopo za umma,” LSK ilisema.
Kulingana na LSK, katiba inampa mamlaka mkaguzi mkuu kukagua deni la umma ndani ya miezi sita baada ya mwisho wa kila mwaka wa kifedha, ikiongeza kuwa hesabu za serikali zote na idara za serikali lazima zikaguliwe na afisi hiyo.
Katika kutetea msimamo wake, LSK ilisema ina jukumu la kulinda na kusaidia umma na kushauri serikali katika masuala yote yanayohusiana na sheria na vile vile kuzingatia Katiba ya Kenya na kuendeleza utawala wa sheria na usimamizi wa haki”.
Rais Ruto aliunda jopo kazi litakalohudumu kwa miezi mitatu – au zaidi — kuanzia leo, Ijumaa 5, 2024, huku sekretarieti yake ikiwa na makao yake makuu katika Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi.