Habari za Kitaifa

Familia kutoka Bonde la Ufa yalaumu kuhama kutoka NHIF hadi SHIF kwa kifo cha mpendwa wao

October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA moja jijini Eldoret, iliyo na wagonjwa watatu wanaougua magonjwa sugu, inasema serikali inafaa kulaumiwa baada ya kifo cha mmoja wa watatu hao aliyekuwa akiugua figo kwa kukosa pesa za kulipa kupata huduma hospitalini.

Kwa familia ya Elizabeth Cheboi, 66, ikiwa bima ya ya afya NHIF ingekuwa inafanya kazi, mama yao angalikuwa hai.

Cheboi alifariki nyumbani kwake katika kijiji cha Chepsiria eneo la Kipchamo, Kaunti Ndogo ya Kesses Jumapili iliyopita baada ya kufukuzwa kutoka hospitali ya Eldoret kwa kukosa pesa za kumsaidia kusafishwa damu licha ya kuwa na kadi yake ya NHIF.

Mmoja wa wanawe ambaye pia anaugua ugonjwa wa figo na kisukari alionyesha kufadhaika kwa familia hiyo kwani watu wengine wa familia moja wameathiriwa na mabadiliko ya hivi majuzi kutoka NHIF hadi SHIF.

‘Ni kama serikali inataka familia yetu yote kufa. Kama NHIF ingalikuwa inafanya kazi, mama yetu asingefariki. Amekuwa akiishi na hali hii kwa miaka 10 iliyopita na amekuwa akipokea dawa kwa hisani ya NHIF,” alisema Simon Bor ambaye anasumbuliwa na kisukari na matatizo ya figo.

Bw Bor alisema juhudi za kujisajili na SHIF zimeambulia patupu tangu Septemba 24.

Alisema licha ya kulipia NHIF kikamilifu kwa miaka miwili ijayo, hawezi kupata matibabu kwa kutumia kadi hiyo kutokana na agizo la hivi majuzi la serikali kuwalazimisha Wakenya wote kuhama kutoka NHIF hadi SHIF.

“Nililipa NHIF miaka miwili mbele nikiwa na matumaini kwamba itanisaidia kupata matibabu lakini sasa haiwezi kunisaidia. Nina hofu baada ya mama yangu kufariki kutokana na kulazimishwa kuhama kutoka NHIF hadi SHIF, bado sijapata thibitisho la usajili niliofanya SHIF,” alisema.

Alikashifu serikali kwa kuwalazimisha Wakenya kuhama kutoka NHIF hadi SHIF bila kuweka njia mwafaka za kuhudumia wagonjwa, haswa wale walio na magonjwa sugu.