Farasi wabakia wawili kwa kiti cha Naibu Rais serikali ikitegea kumpa kisogo Gachagua
MBIO za kumrithi Naibu Rais Rigathi Gachagua iwapo atatimuliwa, sasa ni kati ya farasi wawili, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki.
Taifa Leo imebaini kuwa ni wawili hao ndio wanapigiwa upato wa kujaza nafasi ya Bw Gachagua ambaye hatima yake ipo mikononi mwa seneti.
Baada ya kuondolewa na Bunge la Kitaifa, Seneti Alhamisi itakuwa na nafasi ya kumwokoa Bw Gachagua au kumzika kabisa kisiasa. Wabunge 282 wiki jana waliunga mkono hoja ya kumtimua Bw Gachagua huku 44 wakisimama naye.
Bw Gachagua anaonekana kupoteza imani kwenye Bunge la Seneti kutokana na miegemeo ya kisiasa iliyotumika kupiga kura kumbandua mamlakani kwenye Bunge la Kitaifa.
Akiwa Embu jana, Bw Gachagua alisema kuwa sasa tumaini lake lipo katika mahakama ambako atakuwa akisaka haki baada ya jaribio la kusimamisha kujadiliwa kwa hoja dhidi yake kugonga mwamba.
Kenya Kwanza sasa inatathmini nani kati ya Bw Mudavadi na Profesa Kindiki atachukua nafasi ya Bw Gachagua ambaye amehudumu kwa muda wa miaka miwili na miezi miwili pekee.
Wabunge kutoka Mlima Kenya ambao walimtimua Bw Gachagua wanataka wadhifa huo uendee Profesa Kindiki. Wanaona hilo litawasitiri kwa kuwa mrithi wa naibu rais bado atakuwa akitoka eneo hilo.
Kuelekea hoja ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua, baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya Mashariki walikuwa wametangaza Profesa Kindiki kama msemaji wao. Walimrejelea kama kiongozi ambaye watakuwa wakimtumia kumfikia Rais badala ya Bw Gachagua ambaye walimrejelea kama kiongozi dikteta.
Profesa Kindiki anatoka Kaunti ya Tharaka-Nithi ambayo ipo upande wa Mlima Kenya Mashariki huku Bw Gachagua akitokea Nyeri ambayo ipo Mlima Kenya Magharibi.
“Kutokana na jinsi matukio ya kisiasa nchini yalivyo kuna haja tuwe na kiongozi ambaye atakuwa kiunganishi kati yetu na Rais kuhusu masuala ya maendeleo. Kiongozi huyo ni Profesa Kindiki,” wakasema wabunge huo kupitia taarifa mwezi uliopita.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 kulikuwa na uhasama mkubwa kati ya Bw Gachagua na Profesa Kindiki kuhusu nani alistahili kuwa mgombeaji mwenza wa Rais Ruto.
Profesa Kindiki anaonekana kuwa kifua mbele kuchukua mahala pa Bw Gachagua kwa kuwa kura kadhaa za utafiti zimekuwa zikimweka mbele ya Bw Mudavadi na Kinara wa Upinzani Raila Odinga.
Utafiti ambao ulifanywa na kampuni za Infotrak na TIFA wiki jana zilionyesha kuwa Wakenya wengi wanampendelea Profesa Kindiki awe naibu rais kama Bw Gachagua ataenda nyumbani.
“Waziri huyo wa Usalama wa Ndani anaonekana kama kiongozi ambaye atafanya kazi vyema na wabunge ambao walimtimua Bw Gachagua. Iwapo Mlima Kenya haitapewa nafasi hiyo basi wabunge hao watajipata pabaya kwa kumhangaisha mwanao kisha kupoteza nafasi ya unaibu rais,” akasema afisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka anukuliwe.
“Wale ambao wanamtaka Mudavadi wanasema kuwa yeye ni watatu kwenye itifaki serikalini na hafai kupitwa. Pia wanamwona kama kiongozi ambaye ana uzoefu na uelewaji mpana wa masuala ya serikali,” akaongeza afisa huyo wa serikali.
Wengi ndani ya serikali wanahisi kuwa iwapo Bw Mudavadi atateuliwa naibu rais, basi Profesa Kindiki atapandishwa ngazi kuwa kinara wa mawaziri kwa sababu ndiye kiongozi wa hadhi ya juu sasa kutoka Mlima Kenya baada ya Bw Gachagua.
Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Javas Bigambo amesema kuwa Rais Ruto ana mlima wa kukwea kupata uungwaji mkono Mlima Kenya hata akimpa Profesa Kindiki nafasi ya Bw Gachagua.
“Mbinu pekee ambayo inaweza kumsaidia kwa sasa ni kugawanya kura za jamii ya Kikuyu na kusambaratisha GEMA. Lazima sasa ahakikishe anapata kura za Magharibi mwa Kenya kwa kumteua mwaniaji wake kutoka eneo hilo,” akasema Bigambo.
Mchanganuzi mwengine Richard Bosire naye amepuuza dhana kuwa naibu rais lazima atoke Mlima Kenya kama Bw Gachagua atatimuliwa.
“Hii ndiyo nafasi ya kuwa na naibu rais kutoka eneo jingine badala ya kuwateua viongozi wale wale eti kwa sababu anatoka Mlima Kenya,” akasema Bw Bosire.