Foleni ndefu KICC Wakenya waking’ang’ania kazi za Qatar
MAELFU ya vijana nchini Ijumaa walijitokeza kwa usajili uliotangazwa na serikali wa nafasi za kazi za Qatar.
Foleni ndefu zilishuhudiwa huku kila mmoja akiwa na matumaini ya kupata kazi.
Waziri wa Kazi, Alfred Mutua alitangaza kuwa kampuni ya Qatar ingefanya mahojiano na usajili wa nafasi mbalimbali za kazi mwishoni mwa juma.
Wote waliofika walisimama kwenye foleni iliyozunguka Jumba la Mikutano la KICC.
Serikali ilisema imefanya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo ili kutoa ajira kwa mamia ya Wakenya.
‘Qatar haijawahi kupokea wauguzi au madaktari kutoka Kenya, lakini sasa wamekubali kupata wauguzi na madaktari na wataalamu katika sekta mbalimbali ikiwemo ICT,’ waziri Mutua alisema.
‘Tayari tuna nafasi za kazi 8,000 na matarajio yetu ni kupata angalau watu 3,000 watakaoajiriwa kufanya kazi ng’ambo.”
Joseph Kamore, alisafiri kutoka Nakuru, kujaribu bahati yake. Kufikia saa sita mchana, aliambia Taifa Leo kuwa ni watano tu kati ya thelathini waliohojiwa walikuwa wamekubaliwa, na alikuwa na wasiwasi kwamba kulikuwa na upendeleo.
‘Uchumi hapa ni mgumu,’ akasema.
Anawashauri wale watakaofanikiwa kuwa makini, waaminifu na watumie vyema fursa hiyo.
Brian Ruto alisafiri kutoka Nandi, akiwa na tumaini ya kupata kazi.
“Naamini kuwa mambo yatakwenda sawa. Nitapata kazi,” akasema Bw Ruto.
Kufikia saa saba mchana, alikuwa bado anasubiri mahojiano yake kwa kazi ya udereva.
Kuanzia Ulaya hadi Mashariki ya Kati, serikali imekuwa ikiwatafutia wananchi kazi nje ya nchi ikisema ni hatua ya kupunguza ukosefu wa ajira nchini.
Waziri Mutua ambaye alisema wakati mmoja kwa miaka 15 iliyopita, idadi ya watu wanaotafuta kazi inakua kwa kasi zaidi kuliko uchumi unavyokua, alisema serikali inatafuta ajira za nje kama njia ya kutatua ukosefu wa ajira nchini.
‘Kufanya kazi nje ya nchi kunawapa Wakenya fursa ya kujijenga kifedha na kimaarifa,’ akaeleza Waziri Mutua.
Bw Mutua awali alisema serikali inanuia kuwatafutia Wakenya 5,000 hadi 10,000 nafasi za ajira katika nchi za ng’ambo kila wiki.