Gachagua ajibu Ruto kuhusu madai ya aliitisha Sh10 bilioni
ALIYEKUWA Naibu Rais, Rigathi Gachagua, amepinga vikali madai ya Rais William Ruto kwamba alidai Sh10 bilioni ili kushawishi wapiga kura katika eneo la Mlima Kenya.
Bw Gachagua pia alikanusha madai kwamba alikuwa akizozana na wabunge wa eneo hilo na kuwatisha alipokuwa ofisini akitaja kauli za kiongozi wa nchi kama uongo.
Kupitia anwani yake rasmi ya X punde tu baada ya kauli za rais, Bw Gachagua alisema kwamba tabia ya kudanganya kupindukia ni tishio kubwa kwa taifa.
Gachagua alimshutumu Ruto kwa kusambaza habari za kupotosha na kuwadanganya Wakenya bila kujuta wala kusita.
Akionya kwamba uongo ndani ya uongozi unaharibu imani ya umma na kudhoofisha maendeleo ya taifa, Gachagua alisisitiza kuwa tabia hiyo inapunguza matumaini ya wananchi kwa serikali.
“Sasa nina hakika kuliko wakati mwingine wowote kwamba tabia ya kudanganya kupindukia ni ugonjwa wa akili,” alisema Gachagua.
“Tishio kubwa zaidi kwa nchi yetu ni viongozi kusema uongo waziwazi bila hata kupepesa macho, na kushindwa kwa kiongozi kuoanisha uongo wao na timu yake. Nalilia nchi yangu, Kenya.”
Akizungumza wakati wa mahojiano ya pamoja na vyombo vya habari katika Ikulu ndogo ya Sagana Jumatatu Machi 31, kabla ya ziara yake ya wiki moja katika eneo la Mlima Kenya, Rais Ruto alidai kwamba Gachagua alitaka Sh10 bilioni ili kumsaidia kupata uungwaji mkono katika eneo hilo lenye kura nyingi.
Ruto aliongeza kuwa aliyekuwa Naibu Rais hata alimpa tishio la kumfanya kuwa Rais wa muhula mmoja ikiwa hangekubali ombi hilo.
Hata hivyo, Ruto alisema kwamba alikataa shinikizo hilo, jambo ambalo lilisababisha tofauti kubwa kati yao.
Alidai Gachagua alikorofishana na wabunge, msaidizi wake Farouk Kibet, na hata mwanahabari wa kidijitali Dennis Itumbi.
“Ikanifikia mimi, unajua mimi naweza kukufanya rais wa muhula mmoja, nahitaji bilioni kumi ndiyo niende niongee na watu wa Mlima nikupangie siasa,” Ruto alisema katika mahojiano hayo.
“Nilimwambia sitafanya hivyo. Kama ni muhula mmoja, basi na iwe hivyo kama wewe ndio wa kuamua.”
Kwa mujibu wa Rais, mivutano kati yake na Gachagua ulianza mara tu walipoingia madarakani.
Hata hivyo, Ruto alidai kwamba baadaye Gachagua alianza kutisha wabunge, akiwaambia kuwa kama hawangemtii, wangetimuliwa kabla ya Desemba.
“Na wabunge wakamjibu kwamba kabla ya Desemba, wao ndio wangemshughulikia yeye,” alisema Ruto.