Habari za Kitaifa

Gachagua sasa apata ujasiri wa kumrukia Ruto moja kwa moja

Na GEORGE MUNENE September 29th, 2024 3 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua Jumamosi aliingia kishujaa katika ngome yake ya Mlima Kenya na kumwambia mkubwa wake Rais William Ruto kwamba, hatajiuzulu kufuatia mipango ya kumuondoa mamlakani.

Bw Gachagua alimshutumu Rais Ruto kwa kusukuma wabunge ili kumtimua kutoka serikali ambayo alisema yeye na wakazi wa Mlima Kenya waliwekeza ikafanikiwa kuingia mamlakani na akamwambia akome kumhujumu.

“Rais Ruto akome kuwaambia wabunge waniondoe mamlakani. Ikiwa hahitaji tena kura za Mlima Kenya anafaa kutufahamisha,” alisema Bw Gachagua.

Akizungumza kwa lugha ya Kikuyu aliposimama katika mji wa Ngurubani katika kaunti ya Kirinyaga alipokuwa akielekea Embu na Meru, Bw Gachagua aliapa kwamba, hatasukumwa ili aondoke katika serikali.

“Nilichaguliwa na watu wa Kenya pamoja na Rais na siendi popote,” alisema huku akishangiliwa. Bw Gachagua alimkumbusha Rais Ruto kwamba, walichaguliwa na Wakenya kuwatumikia kwa miaka mitano na anafaa kukoma kumhujumu.

“Rais anafaa kuniruhusu nifanye kazi naye kwa miaka mitatu iliyosalia. Mnamo 2027 ikiwa anataka kuniacha, tutaheshimu uamuzi wake. Kwa sasa tunapaswa kuzingatia kutimiza wajibu wetu kwa sababu Wakenya wanakabiliwa na matatizo mengi ambayo yanahitaji kutatuliwa. Tuna miradi ambayo haijakamilika ambayo ilianzishwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na inapaswa kukamilishwa ili iwafaidi Wakenya. Tuna kazi ya kahawa na chai ambayo haijakamilika. Mimi na Rais tunapaswa kuungana ili kuinua hali ya maisha ya watu wetu,” aliambia umati.

Huku akimtaka Rais kuzingatia maendeleo na sio siasa, sauti kutoka kwa umati ilisikika watu wakisema; ‘usimbembeleze (Rais).’

Bw Gachagua alikariri kuwa, amekuwa mlengwa wa vita vya kisiasa kwa kupigia debe maendeleo ya eneo hilo na kutaka watumishi wa umma kutoka eneo hilo wakome kufutwa kazi.

“Adui zangu wa kisiasa hawafurahii kwa kuwa ninawapenda watu wangu. Wananiita mkabila kwa kuwatetea wakulima wa kahawa na chai. Watu wetu wanatimuliwa serikalini na wanataka ninyamaze,” alisema.

Alidai kuna njama za kugawanya eneo hilo ili kulidhoofisha kisiasa.

“Adui zetu nje ya eneo hili wanajua kwamba, sisi tuna nguvu. Wanataka kuhakikisha tunagawanyika. Ikiwa tutakubali kugawanywa, tutatawanywa kama kinyesi cha nyani. Tunapaswa kukataa mpango huu mbaya,” aliongeza.

Aliwashambulia Wabunge, akiwaambia wamuache ili awatumikie Wakenya.

“Wabunge wamepangwa ili kuniondoa serikalini. Wanapaswa kuzingatia kazi yao ya kutunga sheria ambazo zina manufaa kwa Wakenya na kuniacha mimi na Rais pekee kufanya kazi ya serikali,” alisema Bw Gachagua.

Bw Gachagua alisisitiza kuwa, hajamdhulumu yeyote akishikilia kuwa yuko serikalini na hatabanduka.

“Sina hatia na ninapigwa vita kwa kuwa mkweli. Ikiwa mtu yeyote anadhani nimefanya jambo baya, basi anapaswa kuwaambia watu wa Mlima Kenya ambao walinipigia kura kwa wingi mimi na Rais,” alisema.

Alisema alikuwa katika eneo hilo kuwaambia wakazi wa Mlima Kenya, changamoto anazokabiliana nazo serikalini na jinsi baadhi ya Wabunge kutoka eneo hilo walivyokuwa wakitumiwa kumdhoofisha. Aliandamana na Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu, Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina na Mbunge wa Juja George Koimburi ambao aliwataja kama mashujaa kutoka eneo hilo ambao ‘hawauzi’ watu wao.

Bw Gachagua aliwaambia wakazi kutema Wabunge waliomkataa kama Msemaji wa eneo hilo na kumuidhinisha Waziri wa Masuala ya Ndani Kithure Kindiki.

“Wabunge kama hao ni wasaliti wanaofikiria matumbo yao na hawawezi kuongoza,” alisema.Bi Maina alimhakikishia Bw Gachagua kwamba, wakazi wa Kirinyaga wako nyuma yake kwa asilimia 100 na hapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu wabunge waliomsaliti.

Bi Maina alionya kuwa wabunge wa eneo hilo waliomtenga Gachagua hawatapigiwa kura katika uchaguzi ujao.

Bi Maina pia alimwambia Rais Ruto amtendee haki Bw Gachagua kama Naibu wake ili kuleta amani nchini.

Naye Bw Nyutu alimwambia Rais Ruto azungumze na wabunge ili waachane na mipango yao ya kumuondoa.

“Tunajua Rais ana uwezo wa kukomesha hoja inayopangwa. Anapaswa kuwaambia wabunge waache,” alisema Bw Nyutu.

Alimuomba Rais kuwashirikisha viongozi wa makanisa ili kumpatanisha na Naibu wake kwa utulivu wa nchi.

“Hata kama mtu anataka kuoa mke wa pili, hafukuzi wa kwanza. Rais anapaswa kumuacha Gachagua,” alisema Bw Nyutu.