Gathungu afichua wizi wa mchana katika kaunti
MKAGUZI mkuu wa hesabu za serikali, Nancy Gathungu amefichua ukora unaotumiwa na kuiba pesa kupitia mishahara katika kaunti
Majina yaliyorudiwa, upandishaji vyeo kwa njia haramu na malipo kwa wafanyakazi hewa, ni baadhi ya hila zinazotumika kufyonza pesa za walipa ushuru na maafisa wa kaunti hasa kutoka idara ya fedha.
Kaunti ya Nandi ililipa Sh15.7 milioni kwa vibarua ambao hawakuwa na maelezo kuhusu vituo vyao vya kazi, kibarua walichofanya, siku na kwa muda gani.‘
“Kwa hivyo vibarua huenda walilipwa malipo ya kila mwezi usiolingana na huduma walizotoa kwa serikali ya kaunti na au hakuna huduma zozote zilizotolewa kabisa kwa sababu hakuna rekodi zozote kuhusu kituo cha kazi wala majukumu,” ilieleza ripoti.
Nandi ilimulikwa vilevile kwa kuwapandisha cheo baadhi ya wakurugenzi licha ya kukosa stakabadhi zinazohitajika kwa kazi hizo huku baadhi ya maafisa waliopandishwa cheo wakikabiliwa na masuala ya kinidhamu na uadilifu.
Kaunti ya Siaya, iligunduliwa kuwa na wafanyakazi 20 wanaoshiriki akaunti moja ya benki.Kaunti ya Nairobi ilikithiri kwa ukora ambapo malipo ya mshahara kupitia benki Agosti 2023, yalifichua maafisa 74 walishiriki akaunti moja.
Maafisa 3,216 katika serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Johnson Sakaja walibadilisha daraja la kazi zaidi ya mara moja kwa mwaka huku wengine hadi mara tatu.
Maafisa 197 walibadilisha tarehe za kuzaliwa mara kadhaa, wengine mishahara yao ikiambatishwa nambari tofauti za kitambulisho mara kadhaa kwa mwaka huku wafanyakazi zaidi ya 6,000 wakishiriki akaunti za benki, nambari ya wakala na tawi.
Mombasa, waajiriwa 16 walipandishwa cheo kinyume cha sheria kwa zaidi ya daraja moja bila kupimwa utendakazi wao huku 96 wakiwa wamepitisha umri wa kustaafu lakini wangali kwenye orodha ya mishahara.
Gavana wa Isiolo, Abdi Guyo, aliajiri washauri 36 ikilinganishwa na wanne wanaoruhusiwa, akateua maafisa wakuu 31 dhidi ya 18 wanaohitajika na kuwa na manaibu makarani wawili wa kaunti, wadhifa usiotambuliwa kisheria kuhusiana na wafanyakazi wa kaunti.
Gavana Cicily Mbarire, Embu, aliajiri wafanyakazi 911 lakini makurutu 614 hawakupatikana kwenye orodha ya wanaolipwa mishahara wala watahiniwa walioajiriwa. Maafisa wa kliniki 67 na madaktari 61wanalipwa mishahara lakini hawatekelezi majukumu yoyote katika kaunti ya Machakos.
Wafanyakazi wasiotekeleza majukumu yoyote hawakufanya chochote kati ya Septemba 2023 na Machi 2024.Serikali inayoongozwa na Gavana Wavinya Ndeti vilevile ina wafanyakazi wawili wanaoshiriki akaunti moja na kulipwa Sh487 milioni pesa taslimu.
Samburu iliwalipa wafanyakazi 29 Sh60 milioni chini ya “Kitengo cha Gavana” kisichotambulika kisheria kwenye muundo wa usimamizi wa kaunti na majukumu yao hayakufafanuliwa.