GEN Z WAMECHEZWA? Rais aonekana kutozingatia kikamilifu matakwa ya vijana
KINYUME na matarajio ya wengi, Rais William Ruto ameonekana kutozingatia kikamilifu matakwa ya vijana wa Gen-Z kwa kuwateua tena baadhi ya mawaziri aliowatema wiki jana.
Aidha, miongoni mwa watu 11 aliowateua jana, wamo watatu waliojiuzulu nyadhifa zao za kisiasa baada ya uchaguzi mkuu uliopita walipoteuliwa mawaziri 2022.
Wao ni Mbunge wa zamani wa Garissa Mjini Aden Duale aliyeteuliwa upya kuwa Waziri wa Ulinzi, aliyekuwa Mbunge wa Kandara Alice Wahome (Ardhi) na aliyekuwa Seneta Maalum Soipan Tuya (Mazingira).
Wengine ambao Rais amewateua tena ni Profesa Kithure Kindiki, ambaye amedumishwa katika Wizara yake ya Usalama wa Ndani, aliyekuwa Waziri wa Kawi Davis Chirchir ambaye amemteua waziri mpya wa Uchukuzi na Barabara huku aliyekuwa Waziri wa Biashara Rebecca Miano akiteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Justin Muturi.
Nyuso mpya katika baraza la mawaziri ni; Deborah Baraza (Afya), Julius Ogamba (Elimu), Andrew Muhia Karanja (Kilimo), Magaret Ndung’u (ICT) na Eric Muga (Maji).
Tangu Rais Ruto alipowapiga kalamu mawaziri 21, mnamo Alhamisi wiki jana, isipokuwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, vijana wa Gen-Z wamekuwa wakisisitiza kwamba asiwateue tena bali awalete watu wapya
Aidha, vijana hao, ambao wameungwa mkono na viongozi wa kidini na makundi ya kijamii, walimhimiza kiongozi wa taifa kutowarejesha wanasiasa katika baraza jipya atakaloteua.
“Kwa kuwafuta kazi mawaziri wake, Rais Ruto ameonyesha wazi kuwa hana imani na utendakazi wao. Kwa hivyo, tunataka asirejeshe hata mmoja wao, ateue watu wapya wenye maadili, uwezo, utaalumu na nguvu za kumsaidia kutekeleza matakwa yetu,” akasema Omwansa M. Omwansa, anayesomea shahada ya Uzimili katika Uanasheria katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya.
Na dakika chache baada ya Rais Ruto kutangaza majina ya wateule hao 11, vijana walianzisha kampeni ya, “#Tuonane Tuesday” huku wakielezea kutorishwa na mawaziri hao wapya.
Kauli hiyo imefasiriwa kuwa huenda Gen-Z wakarejelea maandamano Jumanne juma lijalo kupinga awamu hiyo ya kwanza ya mawaziri ambao Dkt Ruto anapania kufanyakazi nao katika serikali ya umoja wa kitaifa (GNU) aliyoahidi kuunda.
Isitoshe, kulingana na matokeo ya kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni TIFA iliyotolewa Alhamisi, asilimia 56 ya watu waliohojiwa walimtaka Rais Ruto asiwarejeshe mawaziri wote waliowafuta kazi.
Kulingana na matokeo ya utafiti huo ulifanywa kati ya Julai 16 na Julai 17, 2024 na kuwahusika watu 1, 570, ni asilimia 24 pekee ya Wakenya walitaka baadhi ya mawaziri wa zamani warejeshewe nyadhifa za uwaziri.
Vile vile, siku moja kabla ya Rais kutangaza mawaziri hao wapya, marais wa zamani wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Nelson Havi na Ahmednasir Abdullahi walisema kufutwa kazi kwa mawaziri 21 wa zamani kunawafanya kutohitimu kuteuliwa upya kwa nyadhifa hizo.
“Mawaziri hao wako katika kundi moja na magavana walioondolewa afisini kupitia kura ya kutokuwa na imani nao au majaji ambao imebainika hawafai kuhudumu tena. Hiyo ndio sheria,” akasema Bw Havi.
Akikubaliana na kauli ya Havi, Bw Abdullahi alisema hivi: “Kwa kuwafuta kazi mawaziri wake, Mheshimiwa Rais alionyesha kutoridhishwa na mienendo na utendakazi wao kwa kiwango kinachokubalika kikatiba. Udhaifu huo haujarekebishwa ndani ya wiki moja iliyopita na hautawahi kurekebishwa siku zijazo.”
Kando na walakini huu, mawaziri hao wapya pia watakumbwa na kiunzi kingine bungeni wakati wa kupigwa msasa kubaini ufaafu wao.
Huenda wakati huu, wabunge haswa wale wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza wasiwe wepesi wa kuwaidhinisha kwa misingi kuwa “wameteuliwa na Rais Ruto”.
Hii ni kutokana na funzo waliopata Juni 25 baada ya vijana wa Gen-Z kuvamia majengo ya bunge kupinga hatua yao ya kupitisha Mswada wa Fedha wa 2024.
Hatimaye Rais alisalimu amri na kuondoa mswada huo uliopendekeza kuongezwa kwa aina mbalimbali za ushuru.