Habari za Kitaifa

Gen Z wamlilia Matiang’i, wamtaka amng’oe Ruto 2027

Na RUTH MBULA, LABAAN SHABAAN June 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

HUKU maandamano yanayoendeshwa na vijana wa Gen Z yakichacha, jina la aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i linatajwa mara kwa mara.

Baadhi ya waandamanaji wanaotumia mitandao ya kijamii, wanamtaka Dkt Matiang’i kujitokeza ili kujiunga nao kupigania uongozi bora na pengine awe Rais wa Kenya 2027.

Vijana hawa wanaashiria kuwa Dkt Matiang’i alikuwa kiongozi aliyefanikiwa zaidi katika mihula miwili aliyohudumu akiwa waziri katika wizara mbalimbali.

“Matiang’i, mambo ni mawili: ujitokeze ama tuje tukuchukue. Tunahitaji uwe rais na si tafadhali,” Naomi Waithira aliandika kwenye mtandao wa X.

Naye Alberto Nyakundi aliandika kwenye mtandao wa Facebook: “Kwa sasa, mtu ambaye anaweza kumbwaga Rais William Ruto 2027 ni Dkt Fred Matiang’i.”

Hata hivyo, mtumiaji mwingine wa Facebook, Ngas Moyiengi, ana maoni tofauti:

“Kuwaona watu hapa wakifikiria kwamba waziri wa zamani Fred matiang’i ndiye mtu anayefaa kwa kazi hiyo kunadhihirisha jinsi watu hawa wasivyojua sababu zao za kukerwa na hali ya kiuchumi,” alisema.

Waandamanaji wameghadhabishwa na serikali ya Rais William Ruto kwa kutetea sera dhalimu za ushuru.

Mjadala kuhusu iwapo Bw Matiang’i ndiye anafaa kuchukua nafasi ya Rais Ruto 2027 uliendelea kupamba moto mtandaoni.

Wanablogu maarufu wa kisiasa kama Bi Pauline Njoroge na Bw Wahome Thuku pia wametumia mitandao ya kijamii, kuashiria kuwa wanatilia mkazo nafasi ya Matiang’i kugombea urais.

Maafisa wachache sana wa umma hupezwa na wananchi baada ya utawala wao kufifia.

Hata hivyo, wanamtandao hao wanamkumbuka Dkt Matiang’i kwa uamuzi wake thabiti na kutokubali kukithiri kwa utepetevu alipokuwa Waziri wa TEKNOHAMA, Elimu na Usalama wa Ndani.

Bidii yake ndiyo ilivutia aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kumkabidhi Wizara ya Usalama wa Ndani na kusimamia utendakazi wa baraza la mawaziri.

Aligongana na Ruto alipokuwa Naibu Rais

Utathmini wa utendakazi wa baraza la mawaziri ulikuwa jukumu la Naibu Rais wa wakati huo William Ruto.

Tukio hili lilimgonganisha na Dkt Ruto lakini akashikilia alikuwa anafanya kazi aliyopewa na mkuu wake.

Na wakati Bw Kenyatta alimuunga mkono Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kuwa Rais, Dkt Matiang’i akamuunga pia.

Wakati wa kampeni, Dkt Matiang’i alinukuliwa na vyombo vya habari akiomba Wakenya wasichague kiongozi yeyote wa mrengo wa Kenya Kwanza.

Alionya kuwa mrengo huu ulijaa wanasiasa mafisadi wasiojali Wakenya.

Lakini, Bw Odinga alibwagwa na Dkt Ruto na hapo Dkt Matiang’i akajikuta njia panda.

Uvumi ukazagaa kuwa serikali mpya ilikuwa tayari kulipiza kisasi. Baadaye makazi yake yakavamiwa usiku na walioaminika kuwa maafisa wa polisi.

Tangu kujiri kwa tukio hili, aliyekuwa waziri hajawahi kuonekana hadharani tena.

Kakaye Dkt Matiang’i, John Matiang’i aliambia Taifa Leo kuwa siku hizi aliyekuwa waziri anafanya kazi na shirika la kimataifa.

“Wiki chache zilizopita alikuwa nyumbani na familia. Familia yake ya karibu na ya mbali zinaishi nchini Kenya. Wakati mwingine yeye hufanya kazi akiwa nyumbani,” alisema kaka yake.

Isitoshe, alieleza kuwa Dkt Matiang’i anafuatilia yanayojiri lakini haoni haja ya kuingilia masuala ya utawala ambao hata haujakamilisha miaka miwili.

Kabla ya kuibuka kwa maandamano ya Gen Z, jina la Dkt Matiang’i lilikuwa vinywani mwa Wakenya.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu waliambia mhadhara wa jamii ya Abagusii kuwa “Dkt Matiang’i ni mmoja wa watumishi bora wa umma katika kipindi hiki.”

“Mnamkumbuka Dkt Matiang’i? Ingawa hatukuelewana kisiasa, alikuwa mtumishi halisi wa umma. Mgala muuwe lakini haki mpe,” alisema Gavana Sakaja.

Magavana pia wamlilia Matiang’i

Magavana Amos Nyaribo (Nyamira) na Simba Arati (Kisii), wamekuwa wakipigia debe kurejea kwa Dkt Matiang’i kwenye ulingo wa kisiasa na hawataki kufikiria kuwa angepotea hivyo.

“Tulikuwa na mtu wetu, Dkt Matiang’i, ninajua atakuja kwa wakati unaofaa. Tutakuwa naye. Tuna viongozi wengine ambao watajibwaga uwanjani 2027. Tumedhamiria kuhakikisha kuwa siku moja, Omogusii (mtu wa jamii ya Abagusii) atakuwa kiongozi wa nchi,” akasema Bw Arati.

Naye Mbunge wa Nakuru Mjini Mashariki Samuel Arama alisema kuwa Dkt Matiang’i anatosha kuwa Rais na ni mmoja wa viongozi wachache sana wanaoweza kubadilisha Kaunti ya Nyamira.

“Nilikuwa wa kwanza kusema kuwa Dkt Matiang’i anafaa kuwania urais badala ya Bw Raila Odinga katika uchaguzi uliopita. Angegombea urais mambo yangekuwa tofauti. Sasa nanadhani anafaa kuja kugombea ugavana Nyamira,” akasema Mbunge Arama katika mahojiano ya hivi majuzi na wanahabari.

Bw Arama alitabiri kuwa Dkt Matiang’i atarejea nchini kufikia Desemba mwaka huu.

Kundi kwa jina ‘Friends of Dr Matiang’i’ linaamini kuwa Dkt Matiang’i anahitajika kutatua matatizo yanayozonga nchi. Kundi hili linajumuisha wataalamu wa jamii ya Abagusii kutoka kote nchini na nje ya taifa pamoja na wanasiasa na viongozi wa dini.

“Ni kweli kwamba baadhi yetu – Friends of Matiang’i– tumekutana na kushinikiza arejeshwe kwa umma,” alifichua mwanachama wa chama hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Aliendelea kueleza kuwa wanachama hao wamemtafuta Dkt Matiang’i na kuagiza waandae mkutano naye ili wamsihi arejee kwenye jukwaa la kitaifa.

“Amekubali kukutana nasi siku zijazo lakini tarehe bado haijabainika,” alisema.

Chama cha United Progressive Alliance (UPA) kilichoshiriki uchaguzi wa 2022, kinachohusiana na Dkt Matiang’i, kilikuwa na mkutano wa wanachama kutoka kaunti za Nairobi, Kajiado na Machakos jijini Nairobi.

Chama hiki kinaongozwa na Gavana Nyaribo na kina wawakilishi wengi katika bunge la kaunti ya Nyamira.

“Katika mkutano wetu, tuliafikiana kwamba tuende kwa aliyekuwa waziri ili arejee katika ofisi ya umma,” alifichua mmoja wa mwanachama wakuu wa UPA. Duru zinaarifu kuwa huenda Dkt Matiang’i akawania ugavana wa Nairobi 2027.