Habari za Kitaifa

Genge Haiti sasa labembelezwa liachilie mwili wa polisi Mkenya

Na NYABOGA KIAGE March 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAZUNGUMZO yanayohusisha serikali na magenge ya Haiti yameanza ambapo viongozi wa magenge hayo wamebembelezwa waachilie mwili wa polisi Mkenya aliyeuawa wiki jana.

Haya yanajiri wakati ambapo familia ya polisi huyo imesema kuwa serikali bado haijawaarifu kuhusu hatima yake, iwapo ameaga dunia au la.
Duru za Kitengo cha Vikosi vya Usalama vinavyodumisha amani nchini humo maarufu kama MSS zilisema mazungumzo yanaendelea ili genge hilo liachilie mwili wa polisi huyo Benedict Kuria Kabiru.

“Juhudi zinafanywa kwa imani kuwa genge hilo litaafikia uamuzi na kuachilia mwili wa polisi huyo. Tayari mazungumzo kupitia njia mbalimbali yameanza,” duru zikaarifu.

Taifa Leo imebaini kuwa genge linalozuilia mwili huo ni Viv Ansanm ambalo linaongozwa na kiongozi hatari wa kuogofya Jimmy ‘Berbecue’ Cherizier, afisa wa zamani wa polisi Haiti.

Kikosi spesheli pia kinaendelea kuvumbua mbinu ambazo zitatumika kupata mwili wa Kabiru ambaye aliaga dunia baada ya mashambulizi ya kushtukiza katika eneo la Pont-Sonde. Alikuwa amesalia tu na miezi minne kabla ya kumaliza kazi yake Haiti.

Hapa nchini, Kabiru alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi Kaskazini mwa Kenya. Mbali na polisi wa Kenya, polisi wengine ambao wanashiriki misheni ya MSS wanatoka Jamaica, Belize, Bahamas, Guatemala, El Salvador na Haiti.

Kikosi cha kuleta amani Haiti kutoka Kenya kinaongozwa na Godfrey Otunge. Ni kaimu Rais wa Haiti Fritz Alphonse Jean ndiye wiki jana alitangaza mauti ya Kabiru akimrejelea kama afisa aliyejituma ili kuhakikisha kuna amani Haiti.

Nchini, familia ya Kabiru eneo la Kiambu jana ilisema kuwa hawajafahamishwa kuhusu mustakabali ya mwanawe.
Philip Kamau, ndugeye marehemu, alisema jana walifanya maombi kwa ajili ya Kabiru lakini hadi sasa serikali haijawaambia chochote kuhusu mauati yake.“Tunaona tu kupitia mitandaoni na vyombo vingine vya habari kuwa ndugu yangu aliaga dunia,” Bw Kamau akaambia Taifa Leo.

“Kwa hakika sitaki kusikia eti ndugu yangu ameaga dunia. Nimeona ikiripotiwa kuwa amekufa lakini huenda serikali ina habari nyingine,” akaongeza Bw Kamau.

Mamake Kabiru, Jacinta Wanjiku wiki jana alisema alikuwa na matumaini mwanawe yupo hai japo bado hawajasemezana tangu iripotiwe kuwa alitoweka na habari za mauti yake kuchipuka.