Habari za Kitaifa

Ghasia Kenya nzima mswada uliosheheni ushuru mpya ukipitishwa

Na WAANDISHI WETU June 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATU kadha waliripotiwa kuuawa na mamia wakajeruhiwa waandamanaji walipomiminika katika barabara za miji yote mikubwa nchini kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Maandamano hayo yaliyofanyika katika kaunti 34 yalifikia kilele baada ya wabunge kupitisha Mswada huo jana alasiri. Vijana walivamia majengo ya Bunge dakika chache baada ya wabunge kupitisha Mswada huo ambao wamekuwa wakiwataka kukataa.

Waandamanaji waliwazidi nguvu polisi na kuvamia majengo ya bunge huku baadhi ya maafisa wakifyatua risasi na kuwaua watu 5 huku majeruhi wakikimbizwa katika hospitali ya Kenyatta kwa matibabu.

Hii haikuwavunja moyo waandamanaji ambao walichoma sehemu ya majengo ya bunge huku wabunge wakilazimika kutorokea katika ofisi zao zilizoko Bunge Towers kupitia njia iliyoko chini ya ardhi.

Waandamanaji waliokuwa na hasira walichoma gari la polisi kwenye barabara ya Parliament kabla ya kuzingira majengo ya Bunge.

Hali ilianza kuchacha jijini Nairobi kuanzia alfajiri baada ya ripoti kusambaa kwamba, wanaharakati saba walikamatwa huku polisi wakimwagwa katikati ya jiji kupiga doria.

Hata hivyo, licha ya kuwarushia waandamanaji vitoa machozi kuwatawanya, hawakutishika huku vijana wakijitokeza kuonyesha hasira zao kufanya shughuli kusimama kote nchini.

Afisi kadhaa za chama tawala za United Democratic Alliance pia zilichomwa huku vijana wakitishia kuvamia makazi na afisi za wabunge waliounga mswada huo.

Afisi ya gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja pia iliteketezwa. Huko Nyeri, maduka yalichomwa baada wabunge kupitisha mswada huo.

Awali, gavana Mutahi Kahiga alikuwa amewaambia vijana wasilegee katika azma ya kuwaondoa “madikteta” ambao alisema wanajaribu kuupitisha mswada huo.

Bw Kahiga ambaye alikuwa akiwahutubia mamia ya waandamanaji aliambia serikali ya Kenya Kwanza imekataa kuwasikiliza vijana na Wakenya wanaopinga mswada huo.

Ujasiri wa kushtua

“Nawashukuru vijana wote ambao wamejitokeza kwa wingi kuonyesha ujasiri wao,” akasema Bw Kahiga.

“Wakenya kamwe wasikubali kuamriwa, hii ni nchi ya kidemokrasia na serikali inapaswa kusikiliza raia wake. Mswada huo unapaswa kutupiliwa mbali,” aliongeza.

Katika mji wa Nanyuki, polisi wa Kaunti ya Laikipia waliwatawanya mamia ya vijana waliokuwa wakiandamana barabarani wakitaka Mswada wa Fedha wa 2024 utupiliwe mbali.

Waandamanaji hao walikabiliwa na polisi walipokuwa wakijaribu kuingia kwa nguvu katika ofisi za NG-CDF za Laikipia Mashariki wakati walinda usalama walipowarushia vitoa machozi.

Hapo awali, maandamano hayo yalikuwa ya amani huku waandamanaji wakipita katika mitaa ya mji, idadi ikiongezeka kwa dakika.

Katika Kaunti ya Meru, waandamanaji waliandamana katika mji wa Meru, Kianjai, Mikinduri, Nkubu na masoko mengine kadhaa wakipinga Mswada uliopendekezwa.

Mamia ya waandamanaji waliokuwa wameandamana na maafisa hao wa polisi waliandamana katika mitaa ya mji wa Meru wakiwa wamebeba mabango.

Huko Kianjai, waandamanaji waliteketeza matairi kando ya barabara ya Meru-Maua na kuleta msongamano wa magari kwenye barabara hiyo yenye shughuli nyingi.

Huko Kirinyaga, walimu wa Shule ya Sekondari ya Vijana walifanya maandamano wakishutumu serikali kwa kupanga njama ya kupunguza pesa zinazotolewa kuwaajiri kwa masharti ya kudumu katika Mswada wa Fedha, 2024.

“Fedha zetu hazifai kupunguzwa hata kidogo, tunahitaji fedha hizo ili tuweze kuajiriwa kabisa,” akasema Bw Josphat Kariuki ambaye ni mwenyekiti wa JSS katika eneo hili. Walisema walimu 46, 000 wa JSS hawataruhusu serikali kuchukua hata senti kutoka kwa fedha zao walizotengewa.

Vile vile, Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Njeri Maina mamia ya vijana waliandamana kupinga mswada huo.

Katika Kaunti za Homa Bay na Embu waandamanaji hao waliteketeza afisi za chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Maandamano hayo pia yaliendelea katika Kaunti ya Kisumu, Siaya, Kakamega, ambapo polisi walikuwa wakitumia vitoa machozi kuwatawanya vijana waliojitokeza kwa wingi kupinga mswada huo wa fedha.